Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 11:21

Kagame: Hatujaomba mtu yeyote kwamba tupeleke wanajeshi wa Rwanda DRC


Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwahutubia wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwa katika mazoezi.
Rais wa Rwanda Paul Kagame akiwahutubia wanajeshi wa nchi hiyo waliokuwa katika mazoezi.

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema kwamba sio lazima nchi hiyo ipeleke wanajeshi wake nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kulingana na mkataba wa viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki.

Kagame amesema kwamba matatizo ya usalama nchini Congo yanaletwa na serikali ya Congo yenyewe na kwamba vita haviwezi kumaliza shida iliyo mashariki mwa Congo

Kagame ana Imani kwamba mzozo wa kiusalama unaondelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unapaswa kutatuliwa kwa njia za kisiasa badala ya matumizi ya nguvu.

Alikuwa akizungumza mjini Kigali wakati Rwanda ikiadhimisha miaka 28 ya vita vya ukombozi wa nchi hiyo.

Nchi za jumuiya afrika mashariki zimekubaliana kutuma kikosi cha wanajeshi kwa ajili ya usalama mashariki mwa Jamhiri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo wanajeshi wa serikali wanaendelea kukabiliana na waasi wa kundi la M23.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imedai kwamba serikali yar ais wa Rwanda Paul Kagame, inahusika kwenye mzozo huo, kwa kuunga mkono na kuwasaidia waasi wa M23.

Rwanda imeanausha madai hayo na badala yake kudai kwamba DRC inaunga mkono waasi wa FDLR wanaotaka kuangusha utawala wa Hagame.

DRC haina Imani na wanajeshi wa Rwanda kuwa katika jeshi la EAC

Kufuatia mzozo huo jumuiya ya nchi za afrika mashariki ambayo Rwanda na DRC ni mataifa wanachama zimeshakubaliana kutuma kikosi cha wanajeshi mashariki mwa DRC, lakini jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeweka wazi kwamba haitaki Rwanda kuwa sehemu ya kikosi hicho.

Rais Kagame ameonekana kutolipa umuhimu mkubwa pendekezo la jeshi la jumuiya ya Afrika mashariki kuingia DRC.

“Kama Jamhuri ya Kimokrasia ya Kongo inasema ina matatizo na ushiriki wa Rwanda kwenye kikosi hicho, mimi sina sina wasiwasi na hilo. Hatujaomba mtu yeyote kwamba tushiriki kwenye kikosi hicho, kama itatokea mtu mwingine na kutoka sehemu nyingine anakwenda pale kwa kuitenga Rwanda lakini akahakikisha analeta suluhu la changamoto hizi, kwa nini niwe na tatizo naye’’ amesema Kagame.

Waasi wa kundi la M23 wameonekana kuwazidi wanajeshi wa serikali ya DRC hasa eneo la mashariki kwa kudhibithi mji muhimu wa Bunagana ulioko katika mpaka wake na Uganda.

Tshisekedi asema M23 sio raia wa DRC

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi alisema mwishoni mwa wiki kwamba wapiganaji wa M23 sio raia wa Kongo isipokuwa wanatoka Rwanda.

Kagame ameonekana mwenye hasira kutoka na kauli ya rais wa Congo, na kuonya kwamba inaweza kuongeza mgogoro na uharibifu mkubwa.

“Kusema kwamba ni watu kutoka Rwanda ni kosa kubwa…hapana hawa ni raia wa Kongo,wamezaliwa Kongo, wameishi Kongo na ndiyo nchi wanayoitambua kama nchi yao asilia, hilo Rais wa DRC analijua wazi ila analikimbia.

Na tatizo hili linapewa uzito na mchanganyiko wa mambo mengi likiwemo hili suala la mipaka iliyochorwa na wakoloni.

Na sasa ukitaka kuwafurusha watu hawa kutoka katika nchi yao, ni vizuri uwafukuze na ardhi yao ambayo wameimiliki kwa miaka mingi’’

Kagame amedai kwamba DRC inasababisha matatizo yake yenyewe

Rais Kagame ameidai kwamba serikali ya DRC ni sehemu ya tatizo la ukosefu wa amani nchini humo, na kuwepo makundi ya waasi kwa sababu sasa imeamua kushirikiana na waasi wa kihutu wa FDLR ambao Rwanda inaendelea kuwalaumu kuendesha mauaji ya kimbari ya mwaka 94.

Rwanda inadai kwamba waasi wa FDLR wanashirikishwa katika jeshi la DRC kupambana na waasi wa M23.

Hata hivyo Kagame amesema kwamba mzozo wa DRC daima hauwezi kutatuliwa kwa vita isipokuwa njia za kisiasa.

“Kuna haja ya kutafuta suluhu la kisiasa kwa raia wa Kongo wanaouzungumza Kinyarwanda wakiwemo hawa wapiganaji wa M23.Lakini hilo ni suala la DRC kulitekeleza na wala siyo mimi.” Amesema Kagame.

Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi wanatarajiwa Angola kwa mazungumzo yanayoongozwa na rais wa nchi hiyo.

Imetayarishwa na Sylivanus Karemera, VOA, Kigali

XS
SM
MD
LG