Wamarekani wanasherekea Thanksgiving siku ambayo utamaduni wake uko katika familia na marafiki wakishirikiana katika kuburudika na vyakula mbalimbali, na hasa nyama ya bata mzinga.
Pia ni wakati wa michezo na kusherekea, ikiwemo maandamano ya siku ya Thanksgiving iliyoanzishwa na maduka ya nguo ya Macy huko New York.
Maandamano hayo ambayo huwavutia watizamaji takriban 200,000, yanakuja, baada ya tukio la wiki kadhaa zilizopita ambapo mhamiaji kutoka Uzbek alituhumiwa kuendesha gari aina ya pick up na kuwagonga waendesha baskeli katika njia yao na kuwauwa watu wanane.
Wakati vyombo vya usalama vimethibitisha kutokuwepo kwa tishio la shambulizi lolote la kuaminika, polisi katika mji wa New York wameweka maelfu ya maafisa katika njia kuu ya maandamano hayo.
Thanksgiving ambayo inaashiria kuanza kwa kipindi cha sikukuu kuelekea Christmas Marekani, inafuatiwa na siku ya “Black Friday” ambapo bidhaa karibuni zote hushushwa bei –ikiwemo nguo, vifaa na vitu vya kuchezea vya watoto.
Sikukuu hii inajulikana kama ni siku muhimu kwa wananchi wa Marekani kwani ni wakati wa kushukuru mazuri na neema zote walizopata kwa kipindi cha mwaka mzima.
Kwa utamaduni wao Wamarekani familia na marafiki hujumuika pamoja na kupika vyakula mbalimbali, kula na kufurahia kwa pamoja.
Siku ya Thanksgiving ilianza katika jimbo la Massachusetts mnamo mwaka 1621.
Kihistoria chanzo cha sikukuu hii inatokana na wahamiaji Wakiingereza ambao baada ya kuwasili Marekani walikuwa wakisherekea pamoja na wenyeji wao mafanikio yao katika uvunaji wa mazao yao na kushukuru juu ya mafanikio hayo.
Mnamo mwaka 1863 Rais Abraham Lincoln aliadhimisha rasmi sikukuu hii ya Thanksgiving na kuifanya iwe ni siku rasmi ya maadhimisho hayo katika dola ya Marekani kila mwaka.