Vijiji hivyo vikiwemo Rwanguba,Kabinti pamoja na Mji wa Bunagana, vilikuwa vimetekwa na waasi hao tangu jumatatu, waliposhambulia kambi za jeshi la serikali.
Waasi hao sasa wanaaminika kuwa kwenye milima ya Chanzu na Runyonyi.
Raia wa Congo wanaendelea kusimulia waliyoyapitia wakati waasi walipoingia mitaa wanayoishi.
“Tangu jana tulikuwa na wasiwasi mkubwa sana. Tulikimbia. Tuliona watu wasio tufahamu. Walikuwa na silaha. Tulikimbia, raia wote walikimbia, tumerudi hapa nyumbani leo hii. Wasiwasi ipo hatujapata usalama tupo bado katika wasiwasi
Tulikimbilia Rwanguba kwenye milima na Busanza na mabondeni chini sana. Tuliwaona kabisa waasi wa M23 kwa macho. Ni wanaume waliovaa vibaya, wasio na sura ya wakongomani. Walikuwa na watoto wachanga waliokuwa na silaha. Wengine wanaweza kuwa na miaka kumi na nne na wengine kumi na tatu, nilivyo waona ndio sababu tuliamua kukimbia kabisa.” Amesema Joseph Anti mkaazi wa Kabinti, Rutshuru.
Wanajeshi wa kulinda amani, wa umoja wa mataifa wanashirikiana na wanajeshi wa DRC kupambana na waasi hao mashariki mwa nchi hiyo.
Imetayarishwa na Austere Malivika, VOA, DRC