Ripoti mpya imeeleza sababu ya mauaji hayo ni kitendo cha uroho wa madaraka kilichowafanya wakishirikiane na kundi la waasi kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Ripoti hiyo iliyotolewa na watafiti wa CRG- Congo Research Group katika Chuo Kikuu cha New York ndiyo yenye maelezo zaidi mpaka hivi sasa juu ya mauaji ya watu zaidi ya 800 na ya kwanza iliyotoa nadharia ya sababu iliyopelekea makamanda hao kufanya mauaji hayo.
Akizungumza na Sauti ya Amerika mkurugenzi wa CRG, Jason Stearns anasema waliwahoji watu wapatao 249, miongoni mwao wale walioendesha mauaji, mashahidi na waathirika pamoja na ripoti za ndani za Umoja wa Mataifa na rikodi za wale waliokamatwa zinazo onyesha kushiriki kwao katika mauaji hayo.
Mamilioni ya watu waliuawa upande wa mashariki ya Congo kati ya mwaka 1996-2003 katika migogoro ya kikanda na dazeni ya makundi ya wapiganaji bado yanaendelea kushikilia maeneo hayo. Lakini mauaji yaliofanyika karibu na mji wa Beni ni ya kikatili mno na yaliyofanyika kwa siri kubwa katika kumbukumbu za hivi karibuni.
Watafiti wa CRG wamewanukuu mashahidi mbalimbali wakisema kuwa makamanda hao wa jeshi , wakiwemo jenerali mstaafu wa ngazi ya juu katika kanda hiyo, alisaidia na katika baadhi ya matukio alihusika katika kuandaa mauaji hayo, ikiwemo kushiriki kwa wanajeshi kuandaa mazingira ambayo wahanga wa mauaji hayo hawataweza kutoroka.
Lakini msemaji wa Serikali ya Congo Lambert Mende amesema maafisa kadhaa wa ngazi ya juu walishahukumiwa kwa makosa yao katika mauaji hayo na kuikosoa CRG kwa kutaka kuibua swala ambalo limekwisha pita.
Jenerali huyo aliyetajwa katika ripoti hiyo, Muhindo Akili Mundos, amekanusha mara kadhaa kuhusika yeye binafsi katika mauaji hayo.
Ripoti hiyo imetoa pendekezo kuwa bunge lichunguze mauaji hayo na jeshi hilo liwekewe vikwazo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi wa watu waliohusika na uvunjifu huo wa amani katika eneo la Beni.