Hivi sasa katiba ya nchi hiyo inaruhusu mihula miwili ya miaka mitano mitano kwa anayegombea urais.
Wakati huohuo maafisa wa ngazi za juu ambao wako katika kamati kuu watakutana siku ya Jumatatu mjini Beijing kujadili suala hilo.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema kuwa iwapo pendekezo hilo litapitishwa Rais Xi Jinping ambaye sasa ana umri wa miaka 64 ataendelea kuongoza taifa hilo baada ya muda kumalizika.
Vyanzo vya habari nchini China vimesema kuwa uvumi umeenea kuwa rais huyo ataongeza kipindi chake cha utawala kupitiliza mwaka 2023. Amekuwa rais wa nchi hiyo tangu mwaka 2013.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema mabadiliko haya kama yatatekelezwa yatakuwa yanakwenda kinyume na katiba.
Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo Xi anatakiwa kuachia madaraka baada ya kumaliza mihula yake miwili.
Wakati awamu ya kwanza ya utawala wake ukifikia kikomo, bila shaka atachaguliwa kuongoza awamu nyingine wakati wa mkutano wa mwaka wa Bunge la nchi hiyo linalojulikana kupitisha viongozi bila kupinga litakalofunguliwa Machi 5, 2018.
Hakuna ukomo katika nafasi yake ya uongozi ndani ya chama na kama jemedari wa majeshi, japokuwa kwa kawaida huwa ni kipindi cha miaka kumi. Alianza kuwa kiongozi wa chama na jeshi Octoba wakati wa kumalizika mkutano mkuu wa chama ambao hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitano.
Kamati kuu wa chama tawala mwaka 2017 kilimpa madaraka zaidi Xi na hivyo amekuwa na nguvu zaidi za kiutawala na kisiasa, kuliko kiongozi yoyote baada ya kuondoka Rais Mao Zedong
Katika mkutano huo maalum wa kamati kuu nadharia za Xi ziliingizwa katika katiba ikiwemo fikra ya kusambaza fikra za ujamaa katika vyuo vikuu mbali mbali nchini China.