Katika hotuba yake kwa viongozi wanaohudhuria kongamano la ASEAN nchini Cambodia, Kishida amesema kwamba ni muhimu kuhakikisha kwamba kisiwa cha Taiwan kina amani na utulivu, kwa maslahi ya usalama wa eneo hilo.
Ameendelea kusema kwamba kuna wasiwasi mkubwa kuhusiana na ukandamizaji wa haki za kibinadamu dhidi ya watu wa Uyghur.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Japan imesema kwamba China imekuwa ikichukua hatua za kichokozi katika bahari ya East China, na zinazoingilia uhuru wa Japan, na kuendelea kuongeza mivutano katika eneo hilo.
Matamshi ya Kishida yanafuatia msimamo wa rais wa Marekani Joe Biden aliyesisitiza kwamba viongozi wa Asia wanastahili kuhakikisha kwamba kuna amani katika kisiwa cha Taiwani na kuhakikisha kwamba kuna uhuru wa usafiri katika bahari ya South China.
Kishida pia amesema kwamba hatua ya Korea Kaskazini kuendelea kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu, ikiwemo kombora lililopaa juu ya Japan, hayakubaliki.