Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 30, 2025 Local time: 10:56

Jaji asitisha maagizo ya Trump ya kusitisha kwa muda misaada ya serikali kuu


Rais Donald Trump akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusaini amri kadhaa za kiutendaji
Rais Donald Trump akizungumza na waandishi wa habari baada ya kusaini amri kadhaa za kiutendaji

Kesi iliwasilishwa Jumanne kwenye mahakama ya serikali kuu jijini Washington kwa niaba ya mashirika yasiyo ya faida, wamiliki wa biashara ndogo ndogo na wataalamu wa afya ya umma, saa chache kabla ya amri ya kusitishwa kwa fedha za ufadhili wa serikali kuu kuanza kutekelezwa.

Msemaji wa White House Karoline Leavitt, katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari, alitetea kusitishwa kwa programu za ruzuku na misaada ndani ya nchi, akiwambia waandishi wa habari ni jukumu la utawala mpya “kuwa msimamizi mzuri wa dola za walipa kodi.”

Leavitt amesisitiza kwamba amri ya Rais Donald Trump haitaathiri programu za misaada kwa watu binafsi, ikiwemo “mafao ya pensheni, mafao ya huduma nafuu ya afya, mafao ya pesa za chakula kwa watu wenye pato la chini, mafao ya ustawi” “na misaada mingine ambayo inapewa moja kwa moja watu binafsi.”

Wademocrats katika Bunge la Marekani wanasema maelezo hayo si sahihi na kwamba kumetokea hali ya taharuki kutokana na amri hiyo ya Trump, ambayo kiongozi wa chama cha Wademocrats kwenye Baraza la Seneti Chuck Schumer, ameitaja kuwa inakiuka sheria, inaharibu, ni hatari na ni ya kikatili.”

“Watu wana hofu kubwa kuhusu amri hiyo,” Schumer aliwambia waandishi wa habari Jumanne alasiri.

Wakati huo huo, Jumanne Jaji alisitisha baadhi ya maagizo ya serikali ya Trump ya kusitisha mikopo ya serikali, ruzuku na misaada mingine ya kifedha, na kuyapa ushindi makundi ya utetezi ambayo yalisema sera hiyo itakuwa na athari mbaya.

Akisikiliza kesi hiyo katika mahakama ya serikali kuu mjini Washington DC, Jaji wa wilaya Loren Alikhan aliamuru utawala wa Trump kutozuia “ruzuku”, au fedha ambazo tayari zilikuwa zimepangwa kutolewa, hadi Februari 3.

Alikhan amepanga kuwa kesi hiyo itasikilizwa tena Jumatatu ijayo ili kuamua hatua zitazofuata.

Forum

XS
SM
MD
LG