Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:10

Ubalozi wa Marekani kuhamia Jerusalem 2019


Makamu Rais wa Marekani, Mike Pence akutana na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem. Jan. 22, 2018.
Makamu Rais wa Marekani, Mike Pence akutana na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem. Jan. 22, 2018.

Ubalozi wa Marekani utafunguliwa mjini Jerusalem kabla ya mwisho wa mwaka 2019, makamu rais Mike Pence amesema.

Makamu rais wa Marekani, Mike Pence amesema Jumatatu kwamba Marekani itauhamisha ubalozi wake nchini Israel kwenye Jerusalem kutoka Tel Avivi mwishoni mwa mwaka 2019.

“Katika wiki kadhaa zijazo, utawala wetu utafanya mpango wa awali wa kufungua ubalozi mjini Jerusalem na ubalozi wa Marekani utafunguliwa kabla ya mwisho wa mwaka ujao,” Pence amesema, akihutubia kwenye bunge la Israel, Knesset, mjini Tel Aviv.

“Jerusalem ni mji mkuu wa Israel, na kama alivyosema, rais Trump ameielekeza Wizara ya Mambo ya Nje kuanza matayarisho ya awali kuuhamisha ubalozi wetu kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem,” ameongezea.

Rais Donald Trump aliondokana na sera ya Marekani kwa kusema Jerusalem ni mji mkuu wa Israel na kuanzisha utaratibu wa kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rex Tillerson awali alisema kuuhamisha ubalozi huo kutachukua miaka kadhaa.

Netanyahu aliwashukuru Trump na Pence kwa kile alichokiita ‘taarifa ya kihistoria’ na kutangaza kwamba uhusiano wa Marekani na Israel ‘haujwahi kuwa wenye nguvu sana.’

Uamuzi wa Trump kuhusu Jerusalem ulikosolewa vikali na viongozi wa wapalestina, akiwemo rais Mahmoud Abbas ambaye alisema Marekani huenda haina tena jukumu katika utaratibu wa amani.

Wabunge wa kiarabu wamesema kuwa watasusia hotuba ya Pence. Netanyahu alikosoa uamuzi huo katika kikao cha baraza lake la mawaziri siku ya Jumapili huku akimuita Pence ni ‘rafiki mkubwa na wake kweli kwa Israel.’

Kabla ya kusafiri kwenda Israel, Pence alikuwa nchini Jordan ambako mfalme Abdullah alielezea wasi wasi wake kuhusu uamuzi wa Jerusalem na kuisihi Marekani “kujenga tena uaminifu na imani’ katika kutafuta suluhisho la mataifa mawili.

Mfalme Abdullah amesema suluhisho pekee kwa mzozo wa waisraeli na wapalestina ni kupatikana kwa suluhisho la muda mrefu la mataifa mawili ambalo limekuwa likizungumziwa na jumuiya ya kimataifa, na Jerusalem Mashariki ni vyema uwe mji mkuu wa taifa la baadaye la Palestina.

Pence amesema nchi hizo mbili zikubaliane kwa kutokubaliana juu ya suala la Jerusalem.

Kabla ya Jordan, Pence aliitembelea Cairo, ambako aliahidi kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Misri katika mapambano yake dhidi ya ugaidi.

Pence pia amekutana na wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo kabla ya kusafiri kwenda Israel.

XS
SM
MD
LG