Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 22:21

Israel inaendelea kushambulia Hezbollah ndani ya Lebanon


Moshi ukifuka kutoka Aramti, karibu na mpaka wa Lebanon na Israel kutokana na shambulizi la Israel dhidi ya kundi la Hezbollah, September 23, 2024.
Moshi ukifuka kutoka Aramti, karibu na mpaka wa Lebanon na Israel kutokana na shambulizi la Israel dhidi ya kundi la Hezbollah, September 23, 2024.

Lebanon ipo katika hali ya machafuko na wasiwasi. Idadi ya watu wanaofariki na wanaokoseshwa makao inaendelea kuongezeka kutokana na mashambulizi makali ya jeshi la Israel yanayolenga wanamgambo wa Hezbollah.

Shirika la umoja wa mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR, limetaja hali nchini Lebanon kuwa ya kutia wasiwasi sana na ya vurugu.

Idadi kubwa ya watu wamekimbilia Beirut na sehemu za karibu, wakitokea kusini mwa Lebanon. Jeshi la Israel limetoa ilani ya kutaka raia kuhama Beqaa Valley.

Kabla ya mashambulizi kuanza, Lebanon ilikuwa na wakimbizi milioni 1.5 kutoka Syria.

Israel, inaendelea kushambulia sehemu ambazo inaamini wanamgambo wa Hezbollah wamejificha ndani ya Lebanon, mpaka wa kaskazini.

Watu wanakimbia kutoka kusini mwa Lebanon wakielekea Beirut, safari ya dakika 90 kwa muda wa kawaida lakini idadi kubwa ya wasafiri imepelekea mlolongo mkubwa wa magari barabarani, na sasa safari inachukua muda was aa 12.

Watu wengine wameonekana mpakani mwa Lebanon na Syria wakijaribu kukimbilia Syria.

Hali hii inatokana na mashambulizi kadhaa ya angani ya jeshi la Israel kuelekea kusini mwa Beirut. Jeshi la Israel IDF limetaja mashambulizi hayo kuwa ya kimkakati na kuahidi kutoa taarifa kamili baadaye.

Shirika la habari la serikali ya Lebanon NNA, limeripoti kwamba mashambulizi yameharibu nyumba.

Shirika la umoja wa mataifa la kuwashughulikia watoto UNICEF, limesema kwamba idadi kubwa ya watoto hawajulikani walipo na kwamba huenda wamefunikwa na mabaki ya nyumba.

Mashambulizi hayo ndio mabaya sana kuwahi kutokea Lebanon tangu mwaka 2006.

Jeshi la Israel limeapa kuharakisha mashambulizi. Mkuu wa jeshila Israel Herz Halevi, amesema kwamba kundi la Hezbollah halistahili kupewa nafasi na kwamba jeshi la Israel litaendelea kufanya kazi kwa nguvu zote akiongezea kwamba oparesheni inahitaji hatua za haraka katika kila sehemu.

Waziri wa afya wa Lebanon Firass Abiad amesema watu 558 wamethibitishwa kufariki, wakiwemo watoto 50 na wanawake 94, katika mashambulizi ya Jumatatu pekee. Hakuna taarifa za uhakika za vifo kutofautisha kati ya raia na wanamgambo wa Hezbollah.

Watu 1,835 wamejeruhiwa katika muda wa siku moja pekee.

Mratibu wa hali ya dharura wa Lebanon Nasser Yassine ameambia waandishi wa habari kwamba watu 16,500 wamekoseshwa makao kufikia wakati tunaandaa ripoti hii, na kwamba shule 150 zinatumika kama makao ya muda katika sehemu mbalimbali Lebanon.

Mapigano yameongezeka zaidi Jumanne

Jeshi la Israel limesema kwamba limemaliza awamu ya pili ya msururu wa mashambulizi dhidi ya Hezbollah ndani ya Lebanon.

Taarifa ya jeshi la Israel imesema kwamba shambulizi la angani limepiga Hezbollah katika sehemu za Beqaa na sehemu zingine kadhaa kusini mwa Lebanon.

Taarifa imeendelea kusema kwamba nyumba iliyokuwa inaweka silaha, kituo cha kupanga mashambulizi na mifumo mingine ya Hezbollha vimeharibiwa. Jeshi limesema kwamba silaha kadhaa zimeharibiwa.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema kwamba kundi la Hezbollah limerusha karibu makombora 100 kuelekea Israel yakilenga Galilee na Haamakin, kaskazini mwa Israel.

Idadi kubwa ya makombora hayo yamenaswa na mifumo ya ulinzi ya Israel lakini kuna nyumba zimeharibiwa.

Kundi la Hezbollah limesema kwamba limevurumisha msururu wa makombora katika mji wa Kiryat Shmona, kaskazini mwa Israel leo Jumanne.

Jeshi la Israel limesema kwamba makombora 50 yameonekana yakivuka kutoka Lebanon yakiingia Israel lakini idadi kubwa ya makombora hayo yamenaswa.

Hezbollah limesema kwamba makombora yake kadhaa kaskazini mwa Israel mapema jumanne, yamelenga uwanja mdogo wa ndege wa kijeshi wa Ramat David, uwanja wa Meggido na uwanja wa ndege za jeshi wa Amos. Viwanja hivyo vyote vya ndege za kijeshi za Israel, vinapatikana karibu na mji wa Afula, kaskazini mwa Israel.

Jeshi la Israel limesema leo Jumanne kwamba mashambulizi yake ndani ya Lebanon yanatokana na hatua ya kundi la Hezbollah kurusha msururu wa makombora ndani ya Israel. Israel imesema imeharibu mifumo 1,600 ya Hezbollah na kwamba baadhi ya silaha zilikuwa zimefichwa ndani ya nyumba za raia.

Athari za mapigano kati ya Israel na Hezbollah

Karibu safari za ndege 40 kuingia na kutoka Beirut zimesitisha safari.

Idadi kubwa za safari zilizositishwa ni ndege zinazowasili Beirut kutoka au kuingia Ujerumani, Saudi Arabia, Umoja wa falme za kiarabu, Uturuko, Ethiopia, Uswizi, Ufaransa, Jordan, Misri, Iraq na Qatar.

Israel imekuwa na migogoro ya miongo mingi na kundi la Hezbollah. Mashambulizi yameongezeka katika miezi ya hivi karibuni tangu Israel ilipoanzisha vita dhidi ya wanamgambo wa Palestina – Hamas. Hii ni baada ya Hamas kushambulia Israel Oktoba 7 mwaka uliopita na kutekeleza mauaji pamoja na kuteka watu nyara.

Hezbollah ni sehemu ya wapiganaji wanaongozwa na Tehran, walio Yemen, Syria, Gaza na Iraq. Wamekuwa wakishambulia Israel tangu vita vya Gaza dhidi ya Hamas vilipoanza.

Israel haijafutilia mbali ripoti za uwezekano wa wanajeshi wake kuingia Lebanon kwa oparesheni dhidi ya Hezbollah.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameambia Lebanon na raia wake kwamba Israel haipo katika vita na Lebanon lakini inapigana na kundi la Hezbollah. Netanyahu ameambia baraza lake la vita kwamba lengo kubwa la Israel ni kusambaratisha nguvu za Hezbollah katika vita vyake na wanamgambo wa Hamas.

Marekani inaamini kwamba Israel au Hezbollah hawana nia ya kuanzisha vita kamili lakini kuna wasiwasi mkubwa kuhusu mkono na ufadhili wa Iran inayounga mkono Hezbollah kwamba Iran inaweza kuingilia kati.

Iran ilionya Israel kwamba italipia gharama ghali kufuatia mashambulizi yake dhidi ya Hezbollah. Rais wa Iran amesema kwamba mashambulizi ya Israel yanaweza kusababisha vita vikubwa mashariki ya kati.

Historia ya mapigano kati ya Israel na Hezbollah

Israel ilichukua karibu nusu ya Lebanon ilipovamia nchini hiyo mwaka 1982. Wanajeshi wa Israel wlidhibithi sehemu kubwa ikiwemo mji mkubwa wa Beirut na kuondoa wanamgambo wa Palestina. Watu 17,000 walifariki katika vita hivyo.

Wapiganaji wa Palestina walipondoka Lebanon, kundi la kiislamu Washia walipewa mafunzo na Iran na kujiingiza katika mgogoro. Walipuaji mabomu ya kujitoa mhanga wenye uhusiano na Washia walishambulia kambi ya wanajeshi wa majini wa Marekani mwaka 1983 na kuua wanajeshi 300, wafanyakazi wa Ufaransa na raia.

Mwaka mmoja baadaye, wapiganaji wenye uhusiano na Iran walipiga bomu dhidi ya ubalozi wa Marekani mjini Beirut na kuua watu 23. Mwaka 1985, wapiganaji waliungana na kuunda kundi la Hezbollah.

Hezbollah ni sehemu ya kundi kubwa la wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran kutoka Yemen,hadi Syria, Gaza, na Iraq ambalo limekuwa likipigana na Israel na washirika wake tangu vita dhidi ya Hamas vilipoanza na wameapa kuendelea kupigana hadi vita vitakapomalizika.

Hali iliharibika zaidi pale Israel iliposema kwamba ilikuwa imemuaa kiongozi wa Hezbollah Fuad Shukur kwa shambulizi la angani mjini Beirut mnamo mwezi July. Hezbollah iliajibu kifo hicho kwa mashambulizi kadhaa ya ndege zisizokuwa na rubani pamoja na makombora kuelekea Israel.

Mapigano yamepelekea maelfu ya watu kukoseshwa makao ndani ya Israel na ndani ya Lebanon, sehemu ya mpakani.

Israel imeapa kwamba lengo lake kubwa ni kuwarudisha makwao maelfu ya watu kwenye mpaka wake wa kaskazini. Zaidi ya watu 100,000 wamekoseswa makao kusini mwa Lebanon.

Forum

XS
SM
MD
LG