Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 08:50

IGP wa zamani Uganda aomba radhi


IGP mpya Okoth Ochola (kushoto) akikabidhiwa ofisi na IGP wa zamani Jenerali Kale Kayihura
IGP mpya Okoth Ochola (kushoto) akikabidhiwa ofisi na IGP wa zamani Jenerali Kale Kayihura

Mkuu wa polisi (IGP) wa zamani nchini Uganda Jenerali Kale Kayihura, ameomba msamaha kwa raia na maafisa wote wa serikali nchini.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa katika hotuba yake ya kukabidhi ofisi kwa mrithi wake Okoth Ochola, Kayihura amesema Alhamisi anaomba radhi kwa makosa yote ambayo huenda aliyafanya wakati akiwa katika madaraka na kusisitiza kwamba anajuta sana.

Kayihura, ameeleza kwamba haikuwa nia yake kumkosea mtu yoyote lakini huenda mazingira ya kazi yalimsukuma kutenda makosa hayo na kuahidi kuendelea kuwa mzalendo kwa taifa.

Generali Kayihura ameomba msamaha na kueleza masikitiko makubwa kwamba katika kulitumikia taifa kwa kipindi cha miaka 12, raia wameyaona makosa yake zaidi kuliko mazuri yake.

Pia amesema huenda hayo yamepelekea kutimuliwa kwake ofisini katika mazingira ya kumfedhehesha.

Kayihura kwa muda mrefu amekuwa akishutumiwa kwa kutumia nguvu dhidi ya wapinzani wa rais Yoweri Museveni hasa Dkt Kiiza Besigye wa FDC.

Polisi wamekuwa wakimshikilia mara kwa mara Bisigye nyumbani kwake chini ya ulinzi mkali, pamoja na tuhuma nyingine za Kayihura kushirikiana na wahalifu kuwadhulumu wanasiasa wengine wa upinzani. Tetesi za kushindwa kukabiliana na wimbi la mauaji hasa wanawake, nazo zimeukabili uongozi wake.

Akitoa hotuba yake ya dakika 30 mbele ya waziri wa ulinzi Jeje Odong, waziri wa mambo ya ndani Obiga kania na waandishi wa habari, Kayihura alionekana mwenye huzuni na kusema kwamba anajuta kwa makosa yote ambayo alifanya akiwa katika madaraka na kuomba msamaha.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC

XS
SM
MD
LG