Idadi ya watu nchini Haiti ambao wameyakimbia makazi yao kutokana na ghasia za magenge imeongezeka mara tatu katika mwaka uliopita na kufikia zaidi ya milioni moja, Umoja wa Mataifa umesema leo Jumanne.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji limesema takwimu zake za hivi karibuni zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 1,041,000 wengi wao wakiwa wameyakimbia makazi yao mara kadhaa, wanataabika kutokana na ongezeko la mzozo wa kibinadamu.
Mwezi Disemba 2023 tulirekodi karibu watu 315,000 waliohamishwa makazi kutokana kwa ghasia, msemaji wa IOM, Kennedy Okoth Omondi aliwaambia waandishi wa habari. Mwaka mmoja tangu wakati huo tumeshuhudia idadi hiyo ikiongezeka mara tatu, na kufikia zaidi ya watu milioni moja ambao hivi sasa wamehamishwa kwa sababu ya ghasia za magenge huko Haiti.
Katika mji mkuu wa Port-au-Prince, IOM inasema watu waliokoseshwa makaazi wameongezeka kufikia asilimia 87 kutokana na vurugu za makundi ya uhalifu, kuporomoka kwa huduma muhimu, hasa huduma za afya na kupelekea ukosefu wa chakula.
Forum