Vifo vimeongezeka baada ya kutokea mfululizo wa milipuko katika kambi za jeshi Equatorial Guinea na kufikia zaidi ya watu 98.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya afya kwa sasa watu walio jitolea wanaendelea kutafuta maiti katika vifusi shirika la habari la Reuters linaripoti.
Takriban watu 615 wamejeruhiwa katika mlipuko wa Jumapili, ambao ulianza na moto katika kambi ya jeshi ya Nkoantoma, katika mji wa bandari wa Bata, kwa mujibu wizara ya ulinzi.
Akimnukuu makamu wa rais wa Teodoro Nguema Obiang Mangue, wizara ya afya imeeleza idadi ya vifo imefikia zaidi ya watu 98, ikiwa ni zaidi ya mara tatu ya idadi iliyokadiriwa awali ya vifo 31.
Kati ya waliojeruhiwa 299 walilazwa hospotalini kwa mujibu wa ujumbe wa Twitter wa wizara ya afya.
Rais Teodoro Obiang Nguema, ambaye ni baba wa makamu wa rais, amezungumzia ajali hiyo kuwa ni uzembe unaotokana na kushughulikia vibaya milipuko.
Ameongeza kwamba mlipuko huo umeharibu karibu nyumba zote, na majengo huko Bata, mji ambao una idadi ya watu 250,000.
Wizara ya afya ya Equatorial Guinea ilitoa ujumbe wa Twitter ambao ulieleza kwamba imeandaliwa timu ya wataalamu wa magonjwa ya akili inayoundwa na wanasaikolojia, madaktari wa akili, na wauguzi ili kushughulikia waathirika wa mlipuko huo.
Picha zilizo chapishwa na vyombo vya habari vya nchini humo zimeonyesha maiti zikiwa zimefungwa katika mashuka na kuwekwa pembezoni mwa barabara, huku watoto wakiwa wametolewa katika Mabaki ya majengo.