Mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC imethibitisha uamuzi wake wa kutomtia hatiani kiongozi wa wanamgambo wa Congo, Mathieu Ngudjolo miaka miwili baada ya kutomkuta na hatia ya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Katika kura ya wingi wa 3 kwa 2 mahakama hiyo yenye makao makuu yake The Hague, ijumaa ilikataa ombi la waendesha mashtaka ambao walitaka kurudiwa tena kwa kesi hiyo. Ngudjolo alishtakiwa katika kuhusika kwake na mauaji ya halaiki mwaka 2003 kwenye kijiji kimoja ambayo yalisababisha vifo vya kiasi cha watu 200 huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC. Waathirika wengi walikufa kutokana na kukatwa mapanga.
Waendesha mashtaka walishutumu kwamba Ngudjolo aliwatumia watoto wanajeshi, alielekeza mashambulizi dhidi ya raia na kwamba walipigana chini ya amri yake, pamoja na ubakaji na vitendo vingine vya utumwa wa ngono.