Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 09:48

ICC yathibitisha kupokea malalamiko ya mauaji ya Kasese


Kasri ya mfalme wa Rwenzori yawaka moto baada ya kukamatwa mfalme Charles Mumbere
Kasri ya mfalme wa Rwenzori yawaka moto baada ya kukamatwa mfalme Charles Mumbere

"Ndugu zetu mlio na jukumu la kulinda usalama, mnapotumwa kufanya kazi, tumieni akili zenu. Wengine mnafanyakazi kazi kama watu waliaocha akili zenu vitandani, " Winnie Kiiza mbunge wa Kasese.

Mahakama ya uhalifu ya kimataifa (ICC), imepokea ombi la wananchi wanaoishi eneo la Rwenzori nchini Uganda, wakitaka rais Yoweri Museveni ashtakiwe kwa mauaji ya zaidi ya watu 100.

Mwandishi wetu wa Kampala, Kennes Bwire ameripoti Jumatano kuwa ICC, imeahidi kuchukua hatua zinazostahiki na itatoa mwelekeo iwapo itafungua kesi dhidi ya Museveni na washauri wake wa karibu.

Malalamiko hayo yanahusisha kuvamiwa kwa ufalme wa Rwenzururu, kuwapiga risasi walinzi wake kadhaa, kuchoma makao ya mfalme, kumkamata mfalme na kuwavua nguo wanawake waliokuwa katika ufalme huo.

Kwa mujibu wa barua kutoka kwa msajili wa mahakama ya ICC, imeeleza kuwa imepokea malalamiko hayo.

Kati ya wale wanaoshutumiwa ni rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kamanda aliyeongoza operesheni hiyo Brigadia Peter Elwelu na Asuman Mugyenyi, ambaye ni mkuu wa shughuli za polisi, kwa mauaji ya zaidi ya watu 100 huko Kasese.

Maelfu ya watu katika wilaya ya Kasese, wakiongozwa na wabunge wao, wanaitaka mahakama ya ICC kuwachukulia hatua hao watu watatu. Lakini serikali imesema haitatishika na itaendelea kuwasaka wanaotaka kuleta uchafuzi nchini.

Japo mahakama ya ICC imeeleza kwamba barua yake haina maana kwamba itaanza uchunguzi moja kwa moja, imesema itasubiri uamuzi wa mahakama.

Serikali ya Uganda

Kwa upande wa serikali ya Uganda msemaji wake, Ofwono Opondo, amesema hatua ya wabunge hao kutaka mahakama ya ICC kuchunguza mauaji ya Kasese ni dalili kwamba wanaolalamika ndio walio na makosa.

Alisisitiza kuwa vyombo vya usalama vya Uganda vinafanya uchunguzi na wakati huo huo kesi hiyo iko mahakamani.

“Uchunguzi unaendelea na washukiwa kadhaa wanaendelea kukamatwa na uchunguzi huo unaendelea kuwafichua washukiwa zaidi,” alisema msemaji huyo.

Mwandishi wa VOA amesema mbunge wa Kasese, Winnie Kiiza amesema: “Ndugu zetu mlio na jukumu la kulinda usalama, mnapotumwa kufanya kazi, tumieni akili zenu. Wengine wenu mnafanya kazi kama watu walioacha akili zenu vitandani.”

“Hufanya kazi wakisema wamepokea amri kutoka juu. Jueni kwamba hata ukitekeleza masharti kutoka juu, utashughulikiwa kivyako,” aliongeza kusema mbunge huyo.

Duru za Habari

Duru za habari nchini Uganda zinadai kuwa wanajeshi walioongozwa na Brigadia Peter Elwelu, walishambulia ufalme wa Rwenzururu mwanzoni mwa i Disemba, na kuwaua zaidi ya watu 100.

Duru hizo zimeeleza kuwa Brigedia Elwelu amesema alipokea masharti ya kushambulia ufalme huo, kutoka kwa rais Museveni aliyekuwa akizungumza naye kwa njia ya simu.

Lakini wanaotaka mahakama ya ICC kuchunguza mauaji hayo ya Kasese, wanasema kwamba mahakama nchini Uganda haiwezi kumchunguza rais na hawaamini kwamba uchunguzi wa vyombo vya usalama una uadilifu wowote.

XS
SM
MD
LG