Marekani na Dunia kwa ujumla inaomboleza kifo cha Barbara Bush aliyefariki jana akiwa na umri wa miaka 92.
Salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi mbalimbali zinaendelea kumiminika kwa familia yake.
Katika taarifa ya maandishi kutoka ikulu ya Marekani -White House, Rais Donald Trump na Mkewe Melania Trump, wamemsifu Barbara Bush kutokana na juhudi zake za kuendeleza kampeni ya watu kujua kusoma na kuandika.
Familia ya Barbara Bush imesema kuwa amefariki kutokana na ugonjwa wa moyo na matatizo ya kupumua, bila kutoa maelezo zaidi.
Mapema wiki hii Barbara Bush aliamua kwamba asipate matibabu zaidi baada ya kulazwa hospitali mara kadhaa hadi kifo chake, amekuwa akipokea huduma ya faraja.
Watu wanaomjua vizuri wamemtaja marehemu kama mtu aliyekuwa mwenye ukali wa maneno na kukosoa , pia kutoa mwelekeo bila uoga.
Alikuwa Mke wa Rais wa 41 wa Marekani George H.W na mama wa Rais wa 43 wa Marekani George W. Bush.
Barbara Bush alihamasisha sana harakati za kusoma na kuandika na kuzindua shirika lisilo la kiserikali, kwa ajili ya kuendeleza harakati za kusoma na kuandika lililojulikana kama Barbara Bush Houston Literacy Foundation linayosimamiwa na Julie Finck.
“Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, amekuwa mama wa taifa wa kusoma na kuandika na kutambuliwa kutokana na juhudi zake za kuimarisha juhudi za watu kujua kusoma na kuandika. Nadhani ari yake ya kutaka watu wajue kusoma na kuandika, imevutia watu wengi kuchangia kufanikisha shughuli za shirika hili,” ameongeza Julie Finck.