Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Novemba 21, 2024 Local time: 09:36

Huldah mzaliwa wa kwanza wa Kenya kujiunga na bunge la Minnesota


Huldah Momanyi Hiltsley akizungumza kutoka ndan i ya jengo la bunge la Minnesota.
Huldah Momanyi Hiltsley akizungumza kutoka ndan i ya jengo la bunge la Minnesota.

Huldah Momanyi Hiltsley aliweka historia hapo Novemba 5 alipokua mhamiaji wa kwanza mzaliwa wa Kenya kuchaguliwa mbunge wa jimbo la Minnesota.

Ameeleza kuwa ushindi wake ni ushahidi kutokana na ustahmilivu, jitihada na kutekeleza ndoto ya kufanikiwa Marekani.

Akisimama ndani ya ukumbi wa jengo la bunge la jimbo hilo kwa mara ya kwanza siku ya kupata maelezo juu ya kazi zake na jinsi mambo yanavyofanyika bungeni, Hiltsley ameiambia VOA kwamba amezidiwa na furaha hana la kusema na ana hamu ya kuanza safari yake kama mbunge.

“Nina furaha kupita kiasi,” amesema Hiltsley. “Leo ni siku ya wabunge wapya kupewa muongozo wa kazi, na mimi kusimama hapa kati kati ya jengo la bunge kama mhamiaji mwanamke mwafrika ni heshima kubwa sana. Kwa hakika nina furaha kupita kiasi nisiyoweza kuielezea.”

Anasema tukio hili la kihistoria halikutokea kwa urahisi. Safari yake hadi bunge la jimbo la Minnesota ilitokana na mapambano magumu ya maisha, ikiwa ni pamoja na kupambana na mfumo wa uhamiaji ambao ulifikia hatua ya kuwarudisha nyumbani familia yake.

Kampeni ya Huldah Hiltsley, Mmarekani mwenye asili ya Kenya akigombania kiti katika mji wa Minneapolis.
Kampeni ya Huldah Hiltsley, Mmarekani mwenye asili ya Kenya akigombania kiti katika mji wa Minneapolis.

Hiltsley anasema asingefanikiwa kufika hapo ingelikua sio uungaji mkono kutoka kwa jamii yake na msaada wa Seneta marehemu Paul Wellstone, aliyemtetea pamoja na familia yake kuweza kupata kibali cha kuishi Marekani, yaani Green Card, na hatimaye uraia.

“Kufikia hapa kwa hakika ni ushahidi wa mapambano ambayo familia yangu imepitia ili kubaki hapa nchini,” amesema Hiltsley.

Ripoti ya VOA ili fungua mlango wa umashuhuri wake nyumbani ambako mara moja vyombo vya habari vya nchi hiyo na vya kimataifa vilianza kufuatilia ushindi wake, huku kukiwepo na sherehe katika kijiji anakotokea baba yake cha Nyamemiso, magharibi mwa mji mkuu wa Nairobi.

Licha ya umashuhuri huo mpya, Hiltsley anaendelea kuwa mnyeneyekevu.

“Mimi ni yule yule msichana kutoka kijiji kidogo cha Nyamemiso kati kati mwa Kenya anaejikuta hivi sasa kwenye vichwa vya habari. Hivyo ningali niko katika kushukuru na kufurahia wasaa huu muhimu,” amesema mbunge mpya wa Minnesota.

Huldah akiwa na kakake
Huldah akiwa na kakake

Huldah Hiltsley anasema ana dhamira ya kuwahamasisha wengine, hasa wasichana nchini Kenya na Marekani kwamba kila kitu kina wezekana.

Anasema yeye ni mfano mwema kwa wanawake na kufanya kazi pamoja ili kuhakikisha kwamba wanafanikwa pia.

Kwa upande wa malengo yake atakapoanza rasmi kazi zake hapo Januari 7, kubwa zaidi ni kutetea masuala yanayohusu zaidi wilaya yake katika mji wa Minnesota. Kipaumbele chake kitakuwa ni pamoja na kuhakikisha usalama wa jamii, kupatikana nafasi za kupata makazi ya bei nafuu, kutetea haki zaidi za wafanyakazi, na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wengi wao katika wilaya yake ni kutoka Afrika.

Forum

XS
SM
MD
LG