Maafisa wa afya wa Gaza wanasema ukosefu wa mafuta imesababisha kusitishwa kazi kwenye hospitali hiyo ambako watoto watano wachanga wamefariki Jumapili pamoja na wagonjwa 7 walokua mahtuti baada ya mashini za kuwapa oxygen kusita kufanya kazi.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo Mohammad Abu Salmiya amesema kwamba kumekuwepo na mapigano katika maeneo yanayozunguka hospitali na kusababisha hofu kubwa miongoni mwa wagonjwa na maelfu ya watu walokimbia huko kupata hifadhi.
Abu Salmiya, anasema wagonjwa wengi zaidi watafariki katika saa zinazokuja pamoja na watoto kadhaa walozaliwa mapema na hakuna umeme kuweza kuwapatia matibabu yanayohitajika.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza na shirika la televisheni ya Marekani CNN, anadai kwamba wapiganaji wa Hamas wanawazuia wagonjwa na watu kuondoka kutoka hospitali hiyo.
Maafisa wa wizara ya afya ya Gaza wanasema mazingira hayaruhusu wagonjwa kuhamishwa na hawajui watawapeleka wapi wakati mashambulizi yanafanyika sehemu zote za Gaza, na kwamba hakuna mpalestina atakae kuwa na imani kuhamishwa na watu wanaowashambulia.
Katika tukio jingine Rais Joe Biden wa Marekani amekuwa na mazungumzo Jumapili na Mfalme wa Qatar Sheik Tamim bin Hamad Al Thani kwa simu, juu ya matukio ya Gaza na juhudi za kuweza kuachiliwa huru kwa wafungwa wote 240 wanaoshikiliwa na Hamas.
Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanayhu amesema kwamba huwenda makubaliano yako karibu kufikiwa ya kuachiliwa huru kwa mateka hao, lakini alikata kutoa maelezo zaidi akihofia kuharibu mipango yao.
Hata hivyo afisa mmoja wa Palestina huko Gaza amemlaum Netanyahu kwa kuchelewesha na kuweka vizuizi ili kuweza kufikia makubaliano ya awali ya kuachiliwa kwa mateka hao.
Kwengineko, Hilali Nyekundu ya Palestina ilieleza Jumapili kwamba vifaru vya Irael vilikua mita 20 kutoka hospitali ya al-Quds mjini Gaza City, na kuzusha hofu na wasi wasi miongoni mwa watu 14,000 wanaojificha huko tangu kunaza mapigano.
Hospitali hiyo ya pili kwa ukubwa imelazimika pia kusitisha kazi zake kutokana na ukosefu wa umeme, na maafisa wanahofia wagonjwa wengi watapoteza maisha yao. Wafanyakazi wa afya wengi katika hospitali hizo wamelazimika kukimbia kwa usalama wao na kuwaacha wagonjwa pekee yao.
Ripoti imetayarishwa kutokana na habari za mashirika ya AFP, Ap, na Reuters
Forum