Rais wa jimbo la Tigray Debretsion Gebremichael ametishia kufanya mashambulizi zaidi akisema watashambulia kituo chochote halali cha kijeshi.
Kiongozi huyo hajasema ni makombora mangapi yaliyo fyatuliwa hapo jana lakini kusisitisha shabaha yao ni mji huo wa Eritrea pekee yake.
Taarifa yake ina thibitisha kuzorota kwa mapigano yaliyoanza huko kaskazini mwa Ethiopia na kuenea katika nchi jirani ya Eritrea.
Kulingana na duru za kidiplomasia roketi tatu zilifyetuliwa hadi Asmara saa chache tu baada ya kiongozi wa Tigray kuonya kwamba huenda akaishambulia Eritrea.
Inaaminika roketi zilikuwa zimelengwa uwanja wa ndege wa mji mkuu wa taifa hilo. Hakuna Habari za uharibifu au majeruhi yaliyo tolewa bado.
Siku ya Jumanne rais wa jimbo ambaye pia ni kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF, aliituhumu Eritrea kwa kupeleka wanajeshi wake kuvuka mpaka na kulisaidia jeshi la taifa la Ethopia.
Tuhuma ambazo Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea Osman Saleh Mohammed amekanusha.
Waatalamu wanasema kwa muda mrefu serikali ya Eritrea imekuwa ikizozana na TPLF, na wanahofia hivi sasa ugomvi wao unaweza kusababisha kuingia katika vita vinavyoendelea kati ya TPLF na Serikali ya shirikisho ya Ethiopia.
Siku ya Jumamosi, serikali ya Tigray ilitangaza kwamba mashambulio ya makombora ndani ya jimbo la Amhara ni ulipizaji kisasi wa mashambulio ya ndege yaliyo fanywa na jeshi la serikali huko Tigry hivi karibuni.
Serikali ya Addis Ababa ilitoa taarifa Jumamosi ikieleza kwamba roketi mbili ziliharibu sehemu ya uwanja wa ndege wa Gondar jimboni Amhara, Ijumaa usiku na moja ikikosa shabaha yake kwenye uwanja wa ndege wa Bahir Dar.
Jeshi la Ethiopia limekuwa likipambana na wapiganaji wa jimbo hilo kwa zaidi ya wiki moja na inaripotiwa mamia ya watu wamefariki tangu Waziri Mkuu Abiy Ahmed kupeleka majeshi yake huko novemba 4.
Mapigano yamesababisha maelfu ya watu kukimbia katika nchi jirani ya Sudan na Eritrea wakidai kuwepo mateso na hali ya wasi wasi.
Mkuu wa kimkoa wa idara ya wakimbizi ya Sudan ya Alsir Khaled amesema Ijumaa kwamba kuna Waethiopia 21,000 waliovuka mpaka wengi vijana waliokuwa na njaa na wamechoka baada kutembea kwa siku kadhaa.