Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 21:47

Hakuna ushuru zaidi kwa unga wa mahindi, ngano, maji ya chupa na pombe nchi Kenya


Kikao cha bunge la Kenya
Kikao cha bunge la Kenya

Raia wa Kenya wamepata afueni kufuatia hatua ya Kamati ya Fedha ya bunge nchini humo kukataa pendekezo la serikali kuongeza ushuru kwenye bidhaa muhimu na za kimsingi hasa unga wa mahindi, mihogo na ngano.

Kamati hiyo imekataa pendekezo la kuongeza ushuru kwa maji ya chupa na pombe, na hivyo basi kutibua juhudi za serikali kuongeza mapato yake ya ziada kupitia ushuru unaolimbikiziwa bidhaa.

Iwapo bunge la Kenya la kitaifa litaidhinisha mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Fedha yanayoghairi pendekezo la serikali kuongeza ushuru kwenye bidhaa muhimu na za kimsingi hasa unga wa mahindi, mihogo na ngano, maziwa na mkate pamoja na kuongeza ushuru kwa maji ya chupa na pombe, basi huenda juhudi za serikali kuongeza mapato yake ya ziada kupitia ushuru unaolimbikiziwa bidhaa hadi shilingi bilioni 50 kuanzia Julai mwaka huu, zikatibuka.

Mapendekezo ya bajeti

Mabadiliko yaliyopendekezwa kwenye Mswada wa Fedha, 2022 huenda yakaifanya gharama ya bidhaa hizi muhimu kusalia ilivyo kwa kiasi kikubwa, iwapo itapitishwa na Bunge kabla ya kuvunjwa kuelekea uchaguzi mkuu.

Wabunge wa Kenya wanasema kuwa kufanya hivyo kutasababisha mfumuko wa bei za bidhaa na kupunguza uwezo wa raia wa Kenya kununua bidhaa hizo, hivyo basi kuongeza gharama za bidhaa na kuyafanya maisha kuwa magumu.

Ripoti ya Kamati hiyo ya Fedha ya Bunge la Kitaifa inayoongozwa na mbunge wa mbunge wa jimbo la Homabay Gladys Wanga, inapendekeza kuwa Wizara ya Fedha iondoe ushuru wa Ongezeko la Thamani wa asilimia 16% kwenye unga wa mahindi na mihogo, mkate na maziwa.

Mapendekezo ya kufadhili bajeti

Ili kuongeza uwezo wake wa kujizolea mapato ya ziada kupitia ushuru, Wizara ya Fedha kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha, ilikuwa imependekeza hatua kadhaa za kulimbikiza ushuru kwa bidhaa hizo kuisaidia serikali ya rais Uhuru Kenyatta kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 2 kufadhili bajeti yake ya shilingi trilioni 3.3 ya mwaka wa kifedha wa 2022/23 ambayo ni ya mwisho kwa utawala wa rais Uhuru Kenyatta, inayokusudiwa kutumika kutekeleza miradi iliyo na uwezo wa kukwamua uchumi wa nchi, kupunguza hali ngumu ya maisha, kupunguza ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, kupunguza viwango vya juu vya umaskini, kutekeleza sera za umma ili kuongeza maendeleo, kupunguza gharama za kufanya biashara, kuboresha mazingira ya biashara, kupanua upatikanaji wa huduma, na kusaidia vijana na wanawake kufikia maendeleo kwa urahisi.

Vipodozi na mapambo ya urembo kutozwa zaidi

Kamati hiyo, hata hivyo, imeridhia pendekezo la Wizara ya Fedha la kuongeza ushuru wa bidhaa za vipodozi na bidhaa za mapambo ya urembo kutoka asilimia 10% hadi asilimia 15.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG