Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 17:31

Google yaambia serikali ya Uganda haiwezi tu kufunga chaneli za You tube


Kampuni ya Marekani ya Google, imeiambia serikali ya Uganda kuwasilisha kesi mahakamani kuhusiana na ombi lake la kutaka kufunga stesheni kadhaa za televisheni zinazopeperusha matangazo yake kupitia You tube.

Serikali ya Uganda kupitia mamlaka ya mawasiliano nchini humo UCC, iliandikia Google ikitaka kampuni hiyo kufunga stesheni ya Ghetto TV na nyingine 13 kwa madai kwamba zimekiuka maadili na kuvunja sheria za upeperushaji habari nchini humo.

Ghetto TV na stesheni nyingine kadhaa, zina uhusiano na chama cha National Unity Platform, chake mgombea wa urais Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Kulingana na vyombo vya habari nchini Uganda, kiongozi wa mawasiliano wa kampuni ya Google barani Afrika Dorothy Ooko, amesema kwamba kampuni hiyo haiwezi kufunga stesheni hizo kwa sababu tu kwamba serikali imetaka ifanyike hivyo.

“Ni vigumu sana kuondoa tu stesheni kwa sababu serikali nataka stesheni hiyo iondolewe kwenye You tube. Tunafuata sheria kila mara, lakini ni lazima iwe amri kutoka mahakamani. Barua zinaonyesha tu yake UCC imewasilisha kwa ubalozi. Sio amri ya mahakama,” amesema Oooko.

Ombi la serikali linajiri wakati kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 14 zinaendelea. Mgombea wa urais Robert Kyagulanyi amepata wafuasi wengi sana kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook na You tube.

Barua ya UCC kwa Google inasema kwamba “tume ya mawasiliano ya Uganda imepokea malalamiko kadhaa kutoka kwa maafisa wa serikali akiwemo waziri wa mambo ya ndani, mwenyekiti wa usalama wa taifa, polisi na jeshi la nchi hiyo kuhusu habari zinazopeperushwa na vituo hivyo vinavyotumia You tube na kwamba vinapeperusha habari ambazo zinavunja sheria ya mawasiliano ya Uganda, ya mwaka 2013 na sheria inayosimamia habari ya mwaka 2019, ibara ya 8 sehemu ya 2.”

Televisheni ambazo zimetajwa kwenye barua ya UCC ni pamoja na TMO Online, Lumbuye Fred, Trending Channel Ug, Uganda Yaffe, Uganda News Updates, Ghetto TV, Busesa Media Updates, Uganda Empya, Map Mediya TV, KK TV, Ekyooto TV, Namungo Media, JB Muwonge na Bobi Wine 2021.

Barua hiyo inadai kwamba televisheni hizo kwenye mtandao wa You tube, zilitumika kueneza machafuko ya hivi karibuni nchini Uganda yaliyopelekea vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG