Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ilisema kwamba Weah alipata asili mia 61.5 ya kura zote zilizopigwa na kupata ushindi kwenye kaunti 14 kati ya 15.
Weah, mwenye umri wa miaka 51, alikuwa anashindana na makamu wa rais Joseph Boakai, kila mmoja akitaka kujaza nafasi ya rais Ellen Johnson Sirleaf, ambaye anaondoka mamlakani baada ya mihula miwili inayoruhusiwa na katiba ya Liberia.
Sirleaf alimshinda Weah kwenye uchaguzi wa mwaka wa 2005, baada ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi kuibuka kutoka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Tume ya uchaguzi ilisema asili mia 56 ya wapiga kura walijitokeza, ambao ni wachache kuliko waliojitokeza tarehe 10 mwezi Oktoba, wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi huo.
Waangalizi walisema kwamba vituo vya kupigia kura wiki hii vilikuwa na utaratibu mzuri kuliko uchaguzi wa oktoba.
Mgombea mwenza wa Weah, Jewel Howard Taylor, ni mke wa zamani wa aliyekuwa rais wa Liberia Charles Taylor, aliyeanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo na ambaye anatumikia kifungo cha miaka 50 nchini Uingereza kwa majukumu yake katika ukatili uliotokea nchini Sierra Leone.
Weah alikuwa mwanasoka mwenye umaarufu mkubwa mnamo miaka ya 90. Alichezea timu kama vile Chelsea, Manchester City na AC milan.