Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 03:06

Gen. Makenga, kamanda mkuu wa M23 amerudi DRC kuongoza mashambulizi


Generali Sultani Makenga, kamanda mkuu wa kundi la waasi la M23 akiwa na walinzi wake katika sehemu ya Mutaho, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. PICHA: REUTERS
Generali Sultani Makenga, kamanda mkuu wa kundi la waasi la M23 akiwa na walinzi wake katika sehemu ya Mutaho, mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo. PICHA: REUTERS

Kamanda mkuu wa kundi la waasi la M23 Generali Sultani Makenga amerudi mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, akitokea nchi Jirani ambayo msemaji wa kundi hilo Maj. Willy Ngoma hakutaja.

Maj. Ngoma amesema kwamba tangu arudi DRC, Generali Sultani Makenga amekuwa akitembelea wapiganaji wake katika sehemu mbali mbali mashariki mwa nchi hiyo ikiwemo katika mji wa Bunagana ambao sasa unadhibitiwa na waasi wa M23.

Makenga, mwenye umri wa miaka 50, anasemekana kujua vizuri nguvu na uwezo wa jeshi la DRC, na eneo zima la kivu kaskazini.

Wachambuzi wanasema kwamba lengo la Makenga ni kutoa maelezo Zaidi kwa wapiganaji wake namna ya kupambana na jeshi la DRC na wanajeshi wa jumuiya ya Afrika mashariki endapo wataingia Congo.

“Bila shaka Generali Sultani Makenga amerudi DRC kutoka kule amekuwa amejificha, ili kuongoza mashambulizi mwenyewe. Amekuwa akiongoza akiwa mbali na sasa yupo na makamanda wake na wapiganaji. Hii ni kuwapa motisha kuendelea kupigana Zaidi.” Amesema Nabende Wamoto mchambuzi wa siasa za maziwa makuu akiwa Kampala, Uganda, katika mahojiano kwenye kipindi cha radio cha kwa undani (saa tatu hadi saa tatu na nusu usiku, Afrika mashariki), idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, VOA.

M23 Wanadhibithi Bunagana, waliwahi kudhibithi Goma

Waasi wa M23 waliwahi kudhibithi mji wa Goma mnamo mwaka 2012 lakini wakalazimika kuondoka kutokana na shinkizo la aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo Barack Obama.

Mkubwa wa General Makenga wakati huo, Generali Bosco Ntaganda, aliyejulikana kama Terminator, na ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 30 katika mahakama ya uhalifu ya kimataifa - ICC, alikuwa amekataa kuamuru wapiganaji wake kuondoka Goma kabla ya aliyekuwa rais wa DRC wakati huo Joseph Kabila, kukubali matakwa ya waasi wa M23.

Makenga, alikataa kumsikiliza Ntaganda na akaamurisha wapiganaji wa M23 kuondoka Goma, hatua ambayo ilimkasirisha Ntaganda.

Uhasama kati ya Generali Sultan Makenga na General Bosco Ntaganda ulipelekea mpasuko katika kundi hilo na kutokea mapigano makali kati ya wapiganaji watiifu kwa kila upande, yaliyopelekea vifo vya wapiganaji kadhaa.

Ntaganda kujisalimisha ICC na hukumu ya miaka 30

Ntaganda, alikuwa sasa kamanda wa kundi la Patriotic forces for liberation of Congo, FPLC. Alikimbia vita hivyo na kuingia Rwanda, ambapo alijisalimisha kwa ubalozi wa Marekani mjini Kigali na baadaye akapelekwa kwa mahakama ya uhalifu wa kimataifa ICC tarehe 22 March 2013.

Ntaganda alipatikana na makosa 5 ya uhalifu dhidi ya binadamu na makosa 13 ya uhalifu wa vita katika eneo la Ituri, mashariki mwa DRC. Alihukumiwa miaka 30 gerezani, Novemba 2019.

Waasi wa M23 walifanya mazungumzo na serikali ya Congo mwaka 2013 ambayo hadi sasa hayajatekelezwa na wanaendelea kudai kutekelezwa kwa mkataba huo wa Nairobi, ikiwemo kuwajumulisha katika jeshi la taifa, kukomesha mapigano ya makundi mengine ya waasi, ukandamizaji wa haki za kiraia, kuwepo utawala bora na ujenzi wa sehemu za mashariki mwa nchi hiyo.

Makenga na kundi lake walizuiliwa Uganda

Generali Sultan Makenga na waasi wa M23 waliwahi kukimbilia Uganda kufuatia mashambulizi makali ya wanajeshi wa umoja wa mataifa, wanaojumulisha wanajeshi wa Tanzania na Afrika kusini baada ya rais Joseph Kabila kuomba msaada wa SADC.

Wakati huo, serikali ya Joseph Kabila ilidai kwamba Uganda na Rwanda walikuwa wanasaidia waasi wa M23.

Waasi hao walikuwa wameteka Bunagana. Na baada ya kukimbilia Uganda na kujisalimisha katika kambi ya jeshi la Uganda ya Bihanga, Kabila aliachana na oparesheni ya kijeshi akiamini kwamba waasi hao walikuwa wameshindwa, lakini walirudi DRC baadaye, kujikusanya na kuanza upya mapigano.

Madai ya DRC kuunga mkono FDLR na Rwanda kuunga mkono M23

Kundi la M23 linadai kwamba waasi wa Democratic forces for the liberation of Rwanda - FDLR wanaotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari katika nchi Jirani ya Rwanda, wanashirikiana na jeshi la Congo na wamepewa vyeo vya juu ndani ya jeshi hilo, madai ambayo DRC inakanusha.

Serikali ya Rwanda vile vile imedai kwamba Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo inaunga mkono waasi hao wa FDLR.

DRC kwa upande mwingine, imedai kwamba Rwanda, inaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imekanusha.

Kuna utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Generali Sultan Makenga, anatoka katika kabila la Watutsi. Alipigana vita vya vilivyoongozwa na Rwanda Patriotic Front – RPF, vilivyomwezesha rais Paul Kagame kuingia madarakani mwaka 1994.

Makenga pia alishiriki katika vita vilivyomuondoa madarakani aliyekuwa rais wa mda mrefu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Mobutu See Seko, na kumueka Laurent Kabila madarakani.

“Generali Makenga ana ujuzi wa mda mrefu katika vita. Ameongoza waasi wa M23 kwa mda mrefu. Alishiriki katika vita vilivyomuondoa madarakani Mobutu See Seko. Anaamini kwamba anapigana vita kwa niaba ya Watutsi. Aliwahi kuripotiwa kwamba ni mgonjwa. Kurejea kwake ni kutuma ujumbe wa serikali ya Congo na viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki kwamba kundi la M23 halipo tayari kuacha vita sasa hadi yale wanayopigania yaheshimiwe. Njia pekee hapa ya kumaliza vita hivi ni kufanya mazungumzo.” Amesema Nabende Wamoto.

Onyo la umoja wa mataifa kuhusu kundi la M23

Wiki iliyopita, maafisa wa umoja wa mataifa walisema kwamba waasi wa M23 wamepata silaha nzito nzito na sasa mwenendo na tabia zao ni sawa na wa jeshi la serikali yenye mpangilio maalum na kwamba waasi hao wana uwezo mkubwa wa kutekeleza mashambulizi makubwa.

Taarifa hiyo imesema kwamba kundi la M23 kwa sasa lina silaha nzito na za kisasa kuliko jeshi la Monusco na la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo

Maafisa wa umoja wa mataifa mjini Goma wanataka baraza la usalama la umoja huo kuimarisha kwa haraka, juhudi zake za kukabiliana na kundi la M23 na kuwapokonya silaha.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG