Taasisi inayoshughulika na viwango vya chakula na dawa Marekani (FDA) inaongeza onyo jipya kwa chanjo ya COVID-19 ya Johnson & Johnson kwa sababu kuhusishwa kwake na hali nadra ya matatizo ya neva.
Taasisi ya serikali kuu inayofuatilia masuala hayo ilitoa taarifa Jumatatu ikisema ilipokea ripoti za awali za watu 100 ambao walipata ugonjwa wa Guillain-Bare baada ya kuchomwa Johnson & Johnson ambayo inatolewa dozi moja pekee.
Kulingana na FDA tatizo la Guillain-Bare linatokea wakati mfumo wa kinga unaharibu seli za neva na kusababisha udhaifu wa misuli na wakati mwingine kupooza. Kati ya watu elfu tatu na elfu sita wanagundulika na hali hiyo kila mwaka nchini Marekani.
FDA ilisema kati ya washiriki 100 wa chanjo ambao walipata ugonjwa wa Guillain-Bare mtu mmoja alikufa na 95 walilazwa hospitali. Kesi nyingi zilizoripotiwa ni za wanaume wenye miaka 50 na zaidi ambapo hali hiyo huwatokea wiki mbili baada ya kuchomwa chanjo.