Katika mahojiano mbele ya Kamati ya Usalama ya Bunge la Marekani Jumatatu, Comey alikanusha madai ya hamasa za kisiasa ya Trump kwamba Rais mstaafu Barack Obama alirikodi simu zake wiki kadhaa kabla ya kuanza uchaguzi.
“Sina taarifa zozote zinazo thibitisha ujumbe wa tweets wa Trump” unaodai kuwa Obama alidukua habari zake huko kwenye Jengo la makao makuu ya Trump (Trump Tower) New York, Comey amesema.
Hata baada ya kutoka tamko hilo la FBI, msemaji wa Ikulu ya White House Sean Spicer ameendelea kusema Trump hataondoa madai yake ya udukuzi wa simu zake.
“Tumeanza mahojiano na bado yanaendelea,” Spicer amesema. “Kuna maeneo kadhaa ambayo yanahitaji kuchambuliwa. Kuna taarifa nyingi ambazo bado zinahitaji kuzungumziwa.”
Comey ameeleza jopo hilo la Bunge kwa kuwa uchunguzi huo dhidi ya ujasusi wa Russia katika kuvuruga uchaguzi wa Marekani ni siri, “ siwezi kusema zaidi nini tunafanya na mwenendo wa nani tunaufuatilia.” Amesema viongozi hao wa wakilishi wa Congress wamepewa muhtasari katika mkutano wa siri.
Lakini Comey amesema kuwa amepewa idhini na Idara ya Sheria kuthibitisha kuwa uchunguzi wa FBI “ unahusisha kuchunguza aina yoyote ya mafungamano kati ya mtu mmoja mmoja anae husika na kampeni ya Trump na serikali ya Russia, na iwapo kulikuwa na mafungamano yoyote kati ya kampeni na Juhudi za Russia za udukuzi.”
Kabla ya mahojiano hayo kufanyika Bungeni, mapema Trump alikejeli kauli yoyote iliyo sema kuwa kampeni yake ilishirikiana na maslahi ya Russia ili kumwezesha kuingia White House, amesema huo ni udhuru “uliotengenezwa” na Wademokrat baada ya kushindwa uchaguzi.
Katika mlolongo wa ujumbe wa Twitter, Trump amesema kuwa James Clapper, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Taifa chini ya Obama, na wengine “ walisha sema hakuna ushahidi” kwamba alishirikiana na Moscow katika kushinda uchaguzi. “Taarifa hii (ya Trump kushirikiana na Russia) ni habari feki,” Trump alitangaza.