Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 17:47

Faini ya hadi Tsh.100,000,000 kwa kukiuka sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi Tanzania


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Aprili 15, 2022
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Aprili 15, 2022

Bunge la Tanzania lilipitisha Mswaada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi mwaka 2022, mapema mwezi Novemba na sasa unasubiri saini ya Rais ili kuwa sheria.

Mswaada unaweka mazingira magumu kwa mtu yeyote anayekusanya taarifa binafsi nchini Tanzania na pia unatoa mamlaka makubwa kwa tume ya kusimamia utekelezaji wake.

Unaweka mazingira magumu kwa wanaokusanya taarifa binafsi nchini Tanzania kuzisafirisha nje ya nchi, pamoja na kutoa adhabu kali ya hadi shilingi milioni 100 na kifungo cha miaka 2 gerezani kwa yeyote atakayekiuka mswaada huo utakapoidhinishwa na kuwa sheria.

Lengo la sheria hiyo ni ulinzi wa taarifa binafsi kwa kuweka kiwango cha chini cha matakwa ya ukusanyaji na kuchakata taarifa binafsi.

Mswaada pia unatoa fursa ya kuanzisha tume ambayo kazi yake itakuwa kulinda taarifa binafsi na kuimarisha ulinzi wa taarifa hizo.

Kulingana na waziri wa habari na teknolojia Nape Nnauye, Mswaada wa taarifa binafsi unalenga kuwalinda wawekezaji.

“Katika dunia ya sasa, wawekezaji hawataki kuwekeza katika nchi ambayo hakuna sheria ya kulinda taarifa zao binafsi. Bila haka kuwepo kwa sheria hii kutavutia wawekezaji wengi hasa katika sekta ya habari na teknolojia.”

Mfano wa taarifa zitakazolindwa na sheria hiyo ni mikataba kati ya kampuni na serikali

Rais Samia Suluhu Hassan akisaini mswaada huo na kuwa sheria, itatumika Tanzania bara na Tanzania Zanzibar.

Yafuatayo ni mambo muhimu yaliyomo kwenye muswada huo

Malengo ya sheria hiyo ni kudhibthi uchakataji wa taarifa binafsi, kulinda faragha za watu kwa kuweka utaratibu wa kisheria kulinda taarifa binafsi.

Anayekusanya taarifa binafsi anahitajika kuhakikisha kwamba taarifa anazokusanya zinapatikana kwa njia halali na taarifa anazokusanya hataziwasilishwa kwa njia tofauti na maudhui.

Tume itakayoundwa itakuwa na jukumu la kulinda taarifa binafsi na kuhakikisha kwamba sheria inalindwa na kutekelezwa, ikiwemo kupokea na kuchunguza malalamiko ya ukiukwaji wa sheria.

Hakuna mtu atakayeruhusiwa kukusanya taarifa binafsi bila kusajiliwa na tume, na atahitajika kwanza kutuma maombi kwa tume hiyo na tume ndiyo iliyo na maamuzi ya mwisho kukubali au kukataa maombi, na endapo hataridhia uamuzi wa kamati, atahitajika kumwandikia waziri wa habari akieleza kero yake. Kipindi cha usajili kitakuwa miaka mitano kuanzia tarehe ya kutolewa cheti cha usajili. Usajili unaweza kufutwa na tume wakati wowote.

Majina ya wakusanyaji wa taarifa binafsi waliosajiliwa na tume yatahifadhiwa katika rejesta maalum.

Kikao cha bunge la Tanzania, Dodoma
Kikao cha bunge la Tanzania, Dodoma

Majukumu ya anayekusanya taarifa binafsi

Kulingana na mswaada huo, mkusanyaji wa taarifa binafsi anastahili kuhakikisha kwamba mhusika anatambua lengo la ukusanyaji wa taarifa binafsi, na kujua wapokeaji wa taarifa binafsi wanaokusudiwa.

Mkusanyaji anatakiwa kutotumia taarifa alizokusanya kabla ya kuhakikisha kwamba taarifa hizo zimekamilika, ni sahihi, zinaendana na maudhui na hazipotoshi.

Mkusanyaji anaruhusiwa kutumia taarifa alizokusanya kwa maudhui mengine iwapo tu mhusika ameidhinisha matumizi yake, matumizi ya taarifa hizo yanakubaliwa kisheria, dhumuni ambalo taarifa binafsi imetumika linahusiana moja kwa moja na dhumuni la ukusanyaji wa taarifa hiyo.

Mkusanyaji wa taarifa binafsi haruhusiwi kufichua taarifa hizo kwa mtu tofauti na mhusika wa taarifa. Haruhusiwi kufanya marekebisho kwenye taarifa alizokusanya bila ya ridhaa ya mhusika na asifute kumbukumbu ya maandishi kama ilivyokuwa kabla ya marekebisho.

Usafirishaji wa taarifa binafsi kwenda nje ya nchi

Tume ina haki ya kuzuia taarifa binafsi zilizokusanywa kutosafirishwa nje ya nchi iwapo itaona kwamba taarifa zilizokusanywa ni muhimu kwa maslahi ya umma. Jukumu kubwa ni kwa mkusanyaji wa taarifa hizo kuelezea umuhimu wa kusafirisha taarifa zilizokusanywa kuelekea nje ya Tanzania.

Na endapo taarifa hizo zinasafirishwa nje ya nchi, mkusanyaji ana jukumu la kuhakikisha kwamba mpokeaji anachakata taarifa binafsi kwa kuzingatia maudhui yaliyopelekea ukusanyaji wa taarifa hizo.

Taarifa zitasafirishwa nje ya nchi iwapo tu ulinzi wa kutosha wa taarifa hizo umehakikishwa katika nchi ya mpokeaji. Utoshelevu wa kiwango cha ulinzi wa taarifa hizo utathminiwa kwa kuzingatia mazingira yanayozunguka usafirishaji, aina ya taarifa, madhumuni na muda wa uchakataji unaopendekezwa. Usafirishaji wa taarifa hizo kutoka Tanzania pia utazingatia sheria katika nchi ya mpokeaji. Maamuzi ya mwisho kuhusu usafirishaji wa habari hizo upo mikononi mwa waziri wa habari.

Waziri wa habari wa Tanzania Nape Nnauye
Waziri wa habari wa Tanzania Nape Nnauye

Mamlaka makubwa kwa tume ya utekelezaji wa sheria

Endapo kula malalamiko ya ukiukwaji wa sheria ya ukusanyaji wa taarifa binafsi, Tume itaanzisha uchunguzi kwa kumuita au kumataka mkusanyaji kufika mbele ya tume, kupokea au kukubali ushahidi dhidi yake kwa kiapo.

Tume ina mamlaka ya kufanya msako katika ofisi za mkusanyaji, kumhoji mtu yeyote, kuondoka na kifaa chochote cha mkusanyaji chenye taarifa binafsi, na tume haitazuiliwa kufanya uchunguzi wake bila kujali sheria nyingine yoyote.

Adhabu kali kwa kuvunja sheria au kukosa kushirikiana na tume

Mtu yeyote atakayezuia tume kutekeleza kazi yake kwa namna yoyote, labda kwa kukosa kutoa msaada kwa tume kufanya kazi yake, atashindwa kutoa msaada au taarifa zilizoombwa na tume, au kutoa taarifa za uongo kwa tume, atapigwa faini ya isiyopungua shilingi 100,000 za Tanzania na isiyozidi shilingi 5,000,000, au kufungwa miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Tume ya utekelezaji pia ina mamlaka ya kutoa notisi kwa mtuhumiwa anapokosa kuzingatia kifungu chochote cha sheria, na endapo notisi hiyo inakosa kuzingatiwa, tume itatoa notisi nyingine ya adhabu itakayoamuliwa na tume hiyo kulingana na uzito wa ukiukwaji na muda ukiukwaji umekuwa ukiendelea.

Tume pia itafanya maamuzi yake kwa kuthathmini iwapo ukiukwaji ulitekelezwa kwa uzembe au kwa nia ya uovu. Kiwango cha juu cha adhabu ni shilingi 100,000,000.

XS
SM
MD
LG