Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 05:54

Facebook imeshitakiwa kwa 'kuchochea vita, kueneza chuki na ubaguzi nchini Ethiopia'


Mumiliki wa kampuni ya Meta Mark Zuckerberg Okt 25, 2019
Mumiliki wa kampuni ya Meta Mark Zuckerberg Okt 25, 2019

Raia wawili wa Ethiopia, wameishtaki kampuni ya Meta inayomiliki mtandao wa Facebook katika mahakama Kuu ya Kenya jijini Nairobi, wakitaka Facebook kuwalipa fidia ya shilingi bilioni 250 waathiriwa wa ujumbe wa chuki na vurugu wakati wa vita vya Tigray nchini Ethiopia.

Walalamishi wanadai kwamba Facebook ilikosa kuzuia ujumbe wa chuki kwenye mtandao wake na kuchochea zaidi vita nchini Ethiopia.

Kesi hiyo inadai kuwa Meta ilishindwa kushughulikia masuala muhimu ya usalama katika mtandao wake huo na haikuwahi kudhibiti ujumbe wa uchochezi uliochapishwa kwenye Facebook na hivyo kuchochea mzozo ulioua maelfu ya watu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia.

Abrham Meareg na Fisseha Tekle, ambao ni watafiti nchini Ethiopia, pamoja na kundi la kiraia la kutetea katiba nchini Kenya Katiba Institute, wameasilisha kesi hiyo mahakamani.

Wanashtumu kampuni ya Meta inayomiliki mtandao wa Facebook kwa ukiukaji mkubuwa wa Katiba ya Kenya wakati wa kuendesha shughuli zake nchini Kenya, Mashariki na Kusini mwa Afrika, kwa kuchangia vurugu kupitia machapisho ya chuki katika mtandao wa Facebook wakati serikali ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed imekuwa ikipambana na waasi na wapiganaji wenye silaha, wa kundi la Tigray People liberation Front TPLF.

Vita kati ya jeshi la serikali kuu ya Ethiopia na kundi la wapiganaji la Tigray, ulianza Novemba 3 2020, wakati waasi hao wa TPLF waliposhambulia kambi ya kijeshi ya Tigray, kaskazini mwa Ethiopia.

Vita hivyo vilisababisha vifo vya maelfu ya watu, na kupelekea kuzuka mzozo mkubwa wa hali ya kibinadamu nchini Ethiopia.

Bango linaloonyesha makau makuu ya kampuni ya Meta, inayomiliki Facebook, Mountain view, California, Marekani. Nove 9, 2022.
Bango linaloonyesha makau makuu ya kampuni ya Meta, inayomiliki Facebook, Mountain view, California, Marekani. Nove 9, 2022.

Ujumbe wa chuki na udhalilishaji

Meareg, Tekle na Katiba Institute, kupitia hati za viapo mahakamani, wanataka kampuni ya Meta (facebook) iwajibike kwa kuchangia vifo vya watu, kuhamishwa kwa familia, kudhalilisha watu binafsi na uharibifu mkubwa katika jamii kwa kushindwa kuzuia machapisho ya maudhui ya uchochezi na chuki kupitia mtandao wake wa Facebook, wakati ina uwezo wa kudhibiti machapisho hayo.

Dudley Ochiel ni wakili wa Katiba Institute.

“wanasema kwamba mitandao ya kijamii vile vile imetumika nchini Ethiopia kuwadhalilisha, wengine wao wakiwa hapa Kenya lakini wamekuwa wakipata ujumbe wa chuki. Kwa hivyo ndio maana tumekuja pamoja tukapeleka hiyo kesi kortini.”

Ujumbe wa chuki , shutuma za ubaguzi wa rangi

Kesi hiyo inadai kuwa tangu mzozo huo uanze nchini Ethiopia, machapisho ya uchochezi na chuki kupitia mtandao wa Facebook yanahusishwa na vurugu na mauaji ya maelfu katika jimbo la Amhara, Tigray na maeneo mengine, na licha kwamba Facebook imeombwa kudhibiti kusambazwa kwa machapisho hayo ya chuki kulingana na kanuni zake za kiusalama mtandaoni, haijachukua wajibu wa kukuomesha usambazaji huo kutoka kwa watumiaji.

Pia, walalamishi hao wanaishtumu Meta kwa ubaguzi wa rangi na sera ambazo zimesababisha uwekezaji mdogo barani Afrika, hasa kwa kushindwa kuwaajiri wafanyakazi wa kutosha wa kudhibiti maudhui kwa lugha za Kiafrika zinazoshughulikiwa na kitovu chake cha Nairobi, kikubwa zaidi barani Afrika.

Hivyo, wanaitaka mahakama kuamuru kwamba Facebook lazima iache kukuza na kusambaza chuki, ipunguze uchochezi wa vurugu, iajiri wasimamizi wa kutosha kudhibiti maudhui kuhudumia masoko ya lugha yanayosimamiwa na kitovu chake cha Nairobi na vile vile kuweka mfuko wa fedha wa kulipa fidia ya shilingi bilioni 250 kwa waathiriwa wa ujumbe wa kuchochea chuki na vurugu katika mtandao wa Facebook wakati wa vita vya Tigray nchini Ethiopia.

Wanajeshi wa serikali ya kitaifa ya Ethiopia wakiwa wamebeba bendera katika hafla ya kuwakumbuka wenzao waliofariki katika mapigano na wapiganaji wa kundi la Tigray Nov 3, 2022.
Wanajeshi wa serikali ya kitaifa ya Ethiopia wakiwa wamebeba bendera katika hafla ya kuwakumbuka wenzao waliofariki katika mapigano na wapiganaji wa kundi la Tigray Nov 3, 2022.

Mbona Kesi imeasilishwa katika mahakama ya Kenya na sio Ethiopia?

Kuwasilishwa kwa kesi hiyo katika mahakama ya Kenya kunatokana na misingi kwamba utumiaji wa kanuni za Facebook unafanyika nchini Kenya na maamuzi ya udhibiti wa maudhui yake yanayoathiri sehemu kubwa ya Afrika vile vile hufanyika nchini Kenya na kwamba Meta hulipa ushuru kwa Serikali ya Kenya hivyo ni shirika la biashara nchini Kenya.

Lakini wakili wa mahakama kuu nchini Kenya Danstan Omari ana tafsiri tofauti.

“Iwapo mahakama ya Kenya itakubali kwamba ina uwezo wa kusikiliza kesi hii, maswali yatakuwa, kitendo kilifanyika wapi? Mtandao wa facebook ulionekana wapi? Kwa hivyo, kesi ifunguliwe mahali kosa lilifanyika. Sidhani kwamba ile kesi imeasilishwa katika mahakama inayofaa, katika taifa la Kenya.”

Hii ni kesi ya pili iliyowasilishwa dhidi ya Meta nchini Kenya baada ya raia wa Afrika Kusini kuishtaki kampuni hiyo kwa mazingira duni ya kazi katika ofisi yake ya Nairobi. Mahakama Kuu ya Kenya ingali kutoa ushauri wa iwapo na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG