Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 02:27

Ethiopia yaomba kujiunga na Jumuiya ya Kiuchumi ya BRICS


Mkutano wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa BRICS mjini Cape Town, Afrika Kusini
Mkutano wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa BRICS mjini Cape Town, Afrika Kusini

Ethiopia, mojawapo ya mataifa yanayokua kwa kasi kiuchumi barani Afrika, imeomba kujiunga na jumuiya ya BRICS ya masoko yanayoibukia, wizara ya mambo ya nje ilisema Alhamisi. 

Neno BRIC lilibuniwa na mwanauchumi wa kampuni ya Goldman Sachs Jim O'Neill mnamo mwaka wa 2001 kuelezea ukuaji wa kiuchumi wa Brazil, Russia, India na China.

Nchi wanachama wa BRIC yalikuwa na mkutano wao wa kwanza mnamo 2009 nchini Russia. Afrika Kusini ilijiunga mwaka 2010, na ndiyo maana herufi ya mwisho ikaongezwa na muungano huo kuitwa BRICS.

"Tunatarajia BRICS itatupatia jibu chanya kwa ombi ambalo tumetoa," msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Ethiopia, Meles Alem, aliwaambia waandishi wa habari, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ENA.

Ethiopia itaendelea kufanya kazi na taasisi za kimataifa ambazo zinaweza kulinda maslahi yake, alisema waziri huyo.

Taifa hilo la pembe ya Afrika linashika nafasi ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika, lakini uchumi wake unashika nafasi ya 59 duniani, kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, na uchumi wake ni chini ya nusu ya ule wa nchi mwanachama wadogo zaidi wa BRICS, Afrika Kusini.

Mwaka jana Argentina, nchi ya 23 kwa uchumi mkubwa duniani, ilisema imepata uungwaji mkono rasmi wa China kujiunga na kundi hilo, ambalo linaonekana kuwa na nguvu kubwa katika soko linaloibukia, kama mbadala wa mataifa ya Magharibi.

Afrika Kusini ilisema Alhamisi itakuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa kilele mwezi Agosti, kama ilivyopangwa, huku kukiwa na uvumi kwamba unaweza kuhamishiwa mahali ambapo Rais wa Russia Vladimir Putin hatalazimika kukamatwa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

Nchi za BRICS zina jumla ya zaidi ya asili mia 40 ya idadi ya watu duniani na karibu asili mia 26 ya uchumi wa dunia.

Forum

XS
SM
MD
LG