Matamshi hayo ya hasira ya Erdogan yanatilia shaka zaidi uwezekano wa Sweden na Finland kujiunga na muungano wa ulinzi wa nchi za magharibi kabla ya uchaguzi wa rais na bunge wa mwezi Mei nchini Uturuki.
Uturuki na Hungary ndizo nchi pekee wanachama wa NATO ambazo hazijaidhinisha uamuzi wa kihistoria wa kuziruhusu Sweden na Finland kujiunga na NATO baada ya kuvunja msimamo wao wa kutoegemea upande wowote kijeshi, kufuatia uvamizi wa Russia dhidi ya Ukraine.
Waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban aliahidi kwamba bunge la nchi yake litaidhinisha miswada miwili mwezi ujao.
Lakini Erdogan amekuwa akisita kuchukua uamuzi wakati uchaguzi unakaribia ambapo anajaribu kuhamasisha wafuasi wa chama chake wenye itikadi ya kihafidhina.
“Sweden isitarajie uungwaji mkono kutoka kwetu ili kujiunga na NATO,” Erdogan amesema katika jibu lake la kwanza rasmi juu ya kitendo cha mwanasiasa anayepinga Uislamu wakati wa maandamano ya Jumamosi ambayo yaliruhusiwa na polisi wa Sweden licha ya pingamizi ya Uturiki.