Macron mwenye siasa za mrengo wa kati alipata asilimia 58 ya kura ikilinganishwa na Lepen aliyepata asilimia 42 kulingana na makadirio ya taasisi za ukusanyi wa kura ya maoni za vituo vya televisheni vya Ufaransa.
Macron ni rais wa kwanza wa Ufaransa kushinda muhula wa pili kwa miongo miwili, lakini matokeo ya Lepen pia yanaashiria kuwa chama cha mrengo mkali wa kulia kimekaribia sana kuchukua madaraka nchini Ufaransa na yamefichua kwamba taifa hilo limegawanyika sana.
Rais Macron mwenye umri wa miaka 44 anakabiliwa na msururu wa changamoto katika muhula wake wa pili, kuanzia uchaguzi wa wabunge mwezi Juni, ambapo kushikilia viti vingi bungeni itakuwa na umuhimu mkubwa ili kuhakikisha kwamba anaweza kutimiza malengo yake ya kuleta mageuzi nchini Ufaransa.
Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa leo Jumatatu.
Katika hotuba yake ya ushindi kwenye barabara ya Champ de Mars, katikati mwa mji mkuu Paris, chini ya mnara wa Eiffel, Macron amepania kutoa jawabu kwa hasira ya wapiga kura waliomuunga mkono mpinzani wake wa mrengo wa kulia, akisema muhula wake mpya hautaendelea bila kubadilika kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita.
“Jibu lazima lipatikane kwa hasira na kutoelewana ambako kumepelekea wenzetu wengi kupigia kura chama cha mrengo mkali wa kulia. Litakuwa jukumu langu na la walio karibu nami,” amewambia maelfu ya wafuasi waliokuwa wakishangilia.