Gavana wa Kivu kaskazini Julien Paluku ameiambia VOA Jumatano kwamba vipimo vya wakazi wa mtaa wa Mangina waliokuwa na dalili za ugonjwa huo ikiwemo kuharisha na homa kali, vilitumwa Kinshasa Jumatatu na vimethibitshwa kuwa na virus vya Ebola.
Kwa mjiibu wa Gavana Paluku, serikali ya mkoa imetangaza hali ya tahadhari katika jimbo la Beni na vitongoji vyake ili kuzuia ugonjwa huo usiendelee kusambaa.
Pia wanainchi wametahadharishwa kutoondoka katika maeneo yao na kwamba serikali inatuma ujumbe wa watalamu wa afya kutoka Kinshasa kwa ajili ya kuleta vifaa maalum vya kukabiliana na maradhi hayo, na kuandaa mikakati maalum wa kuwasaidia wananchi kukabiliana na hali hiyo.
Gavana Paluku amesema kwamba serikali inayo madawa na chanjo, lakini imeomba washirika wa afya duniani ikiwemo shirika la afya duniani (WHO) kuendelea kuwasaidia katika kukabiliana na mlipuko huo mpya wa Ebola.
Ebola imetokea kivu kaskazini, wiki moja baada ya serikali ya DRC kutangaza kwamba ugonjwa huo uliojitokeza mwezi Mei katika jimbo la Equateur ulizimwa baada ya kuuwa watu zaidi ya 30.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC