Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 21:09

Dubai: Watetezi wa sekta ya mafuta, gesi na makaa ya mawe wahudhuria kwa wingi mkutano wa COP28


Maandamano kupinga matumizi ya uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi ambavyo wanaharakati wa mazingira wanataka visitishwe uzalishaji wake kabisa, yaliofanyika katika mkutano wa hali ya hewa COP28, Dubai, UAE.
Maandamano kupinga matumizi ya uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi ambavyo wanaharakati wa mazingira wanataka visitishwe uzalishaji wake kabisa, yaliofanyika katika mkutano wa hali ya hewa COP28, Dubai, UAE.

Wanaharakati wa hali ya hewa wanasema idadi kubwa ya watetezi kutoka katika sekta ya mafuta, gesi na makaa ya mawe wanahudhuria mkutano wa hali ya hewa wa COP28 huko Dubai.

Wakati huo huo mazungumzo kadhaa yameshika kasi kujadili iwapo dunia iazimie kukamilisha kusitisha kabisa uchimbaji makaa ya mawe, mafuta na gesi.

Takriban wajumbe 70,000 wanahudhuria COP28, kati yao ni wakuu wa nchi, wanasiasa, wanasayansi na wanaofanya kampeni – wote wakishawishi maslahi kadhaa na fikra mbali mbali.

Licha ya ugumu wa masuala hayo, mkutano huo unaelekea umejikita kushughulikia suala moja muhimu: Je, kuna umuhimu wa kupiga marufuku nishati ya asili chafuzi mara moja?

Sababu za Ongezeko la Joto Duniani

Makaa ya mawe, mafuta na gesi vinalaumiwa kwa sehemu kubwa ya kuongezeka kwa joto duniani lakini pia ni nguvu inayoendesha uchumi sehemu nyingi duniani, ikiwemo uchumi wa wenyeji wa mkutano huo Umoja wa Falme za Kiarabu.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha mwaka 2023 unatarajiwa utakuwa ni mwaka wa kuvunja rekodi kwa ongezeko la gesi chafu ya carbon dioxide, ikikadiriwa kuenea kwa tani 36.8 bilioni za metriki za CO2 zikitokana na mafuta, gesi na makaa ya mawe yanayochomwa, na iliyobakia ni katika ukataji wa miti na mabadiliko ya matumizi ya ardhi, kulingana na utafiti kutoka Mradi wa Global Project.

Ongezeko la Gesi Chafu

Ongezeko la gesi chafu kila mwaka linahusika na mabadiliko ya hali ya hewa yetu. Na endapo hatua hazitachukuliwa kudhibiti hili kufikia sifuri, basi joto hilo litaendelea,” Corinne Le Quere, mwanasayansi wa mazingira katika Chuo Kikuu cha East Anglia, ameliambia shirika la habari la AP.

Utafiti kutoka taasisi ya Kick Big Polluters Out – muungano wa vikundi vya wanamazingira wanaohudhuria COP28 – wanaeleza zaidi ya wajumbe 2,400 wanahudhuria mkutano huo wana muingiliano na viwanda vya nishati asilia ya fossil.

“Hii ni mara saba zaidi ya wajumbe kuliko wazawa, na ongezeko la mara nne ukilinganisha na mkutano wa mwaka jana uliokuwa na wajumbe 636 waliokuwa wapambe kutoka katika viwanda vya nishati asilia [kwenye COP27],” amesema Eric Njuguna, mwanachama wa kikundi cha Fridays for Future campaign ambacho ni sehemu ya muungano huo.

Makubaliano ya Paris

Wanasayansi wanasema gesi chafu ya viwandani lazima ipunguzwe kwa asilimia 43 katika kipindi cha miaka sita ijayo iwapo dunia inataka kufikia lengo la Makubaliano ya Paris la kudhibiti ongezeko la joto kufikia nyuzi digrii 1.5 Celsius juu ya viwango vilivyokuwepo kabla ya kuwepo viwanda, kwenda juu zaidi wanasema mabadiliko ya hali ya hewa yatakuwa ni janga na haliwezi kudhibitiwa.

Hata hivyo, makadirio ya hivi sasa yanaonyesha ongezeko la gesi chafu litafikia asilimia 9 ikilinganishwa na kipindi kama hicho.

“Na ndio maana katika COP28, tunahitaji dhamira yenye nguvu kuondoa aina zote za nishati chafuzi – siyo tu makaa ya mawe, siyo tu nishati ya mafuta na gesi, lakini aina zote za nishati chafuzi – ikiwemo mafuta, gesi na makaa ya mawe,” Njuguna ameiambia VOA.

Ripoti ya mwandishi wa VOA Henry Ridgwell.

Forum

XS
SM
MD
LG