Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 05:00

DRC na Rwanda zajibizana kuhusu waasi wa M23


Wanajeshi wa DRC wakiwa katika harakati za kupambana na waasi wa M23. (Picha na Austere Malivika)
Wanajeshi wa DRC wakiwa katika harakati za kupambana na waasi wa M23. (Picha na Austere Malivika)

Serikali ya Rwanda imekanusha taarifa zilizotolewa na jirani yake Jamhuri ya kidemokorasia ya Congo kwamba inawaunga mkono waasi wa M23 ambao wameripotiwa kushambulia kambi ya jeshi, kutoroka na silaha na kutekeleza mashambulizi.

Jeshi la DRC limedai kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi hao kutekeleza mashambulizi dhidi ya kambi za jeshi mashariki mwa nchi hiyo, eneo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni na msemaji wa jeshi la CONGO Brigedia Sylvain Ekenge, jeshi la DRC lilisema kwamba “waasi wa M23, kwa msaada wa jeshi la Rwanda, walishambulia kambi za jeshi la FARDC za Tchanzu na Runyonyi, usiku wa tarehe 27 na 28 mwezi March.”

Idadi ya wanajeshi wa DRC waliouawa katika shambulizi dhidi ya kambi zao haijajulikana.

Rwanda yajibu DRC

Serikali ya Rwanda, imetoa taarifa jumanne, ikitaja madai hayo kuwa “si ya kweli”, ikiongezea kwamba “Kigali haijihusishi kwa namna yoyote na mashambulizi ya waasi hao nchini DRC.”

Taarifa ya jeshi la DRC imesema kwamba wanajeshi wawili wa Rwanda wamekamatwa na jeshi la DRC katika makabiliano.

Wanajeshi hao wametajwa kuwa “Jean Pierre Habyarimana mwenye namba za usajili AP 27779 NA John Muhindi Uwajeneza, wote kutoka kikosi cha 65 cha jeshi la Rwanda.” Rwanda inasema kwamba “haina mwanajeshi yeyote na majina kama hayo katika kikosi chake.”

Serikali ya Rwanda vile vile imedai kwamba watu hao wawili walioasilishwa na jeshi la DRC kwa waandishi wa habari, “waliwahi kuwasilishwa wakati wa kikao cha maafisa wa ujasusi kati ya DRC na Rwanda, Februari 28 mwaka 2022.”

DRC yatoa ‘ushahidi’

Jeshi la DRC hata hivyo linasisitiza kwamba “wanajeshi hao wawili ni wanajeshi wa Rwanda na kwamba kamanda wao ni Lt. Col. Joseph Rurindo na Generali Eugene Nkubito, kutoka kambi ya kijeshi ya Kibungo nchini Rwanda.”

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha muda mrefu, Jeshi la DRC linaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi wa M23, wenye nia ya kuvuruga utulivu mashariki mwa DRC.

Kundi la M23 liliundwa kutoka kwa kundi lililokuwa likiongozwa na Generali Bosco Ntaganda, la CNDP.

Vita vya M23 vilianza mwaka 2012 na kuendelea hadi mwaka 2013 baada ya kuvunjika kwa mkataba wa amani na serikali ya DRC. Wapiganaji wa kundi hilo walikimbilia Uganda baada ya kuzidiwa na oparesheni ya kijeshi yaliyoongozwa na wanajeshi wa Tanzania, Malawi, DRC na Afrika kusini.

Katika Oparesheni hiyo, Afrika kusini ilikuwa ikitoa habari za ujasusi huku wanajeshi wa Tanzania wakitumia roketi dhidi ya waasi hao wa M23 na kuwalazimu kukimbia kambi zao na kuingia Uganda na Rwanda.

Baadhi ya waasi hao walirudi DRC kwa hiari huku wengine wakiamua kubaki katika kambi ya jeshi la Uganda ya Bihanga, magharibi mwa Uganda.

Kiongozi wa kundi hilo Sultani Makenga anaaminika kurudi DRC na badhi ya vyombo vya habari vimeripoti kwamba anaongoza mashambulizi mapya.

Ushirikiano kati ya Rwanda na DRC dhidi ya waasi

Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo zilishirikiana katika oparesheni ya kijeshi miaka miwili iliyopita katika kukabiliana na makundi ya waasi nchini Congo.

Lakini Brig Ekenge amesema katika taarifa kwamba “wana taarifa za kuaminika sana kwamba Rwanda inaunga mkono waasi hao na kusema maana ya ushirikiano na jirani aiyeheshimu maneno na ahadi zake katika mikutano kadhaa ambayo imefanyika.”

Rwanda inasisitizwa kwamba “DRC na Rwanda zina mbinu za kuthibitisha madai ya aina yoyote chini ya ushirika wa nchi za maziwa makuu ICGLR, na ushirikiano wa baina ya nchi ili kuthibitisha madai hayo na kwamba DRC ingetumia njia hiyo mara moja iwapo walikuwa na nia nzuri.”

Rwanda sasa inataka DRC kuchunguzwa kutokana na shutuma zake dhidi ya Rwanda

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG