Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 08:02

DRC: Hatuwezi kufanya mazungumzo na M23, ni ‘magaidi’


Wanajeshi wa serikali ya DRC wakipigana na waasi wa M23 karibu na Matebe, Kivu, mashariki mwa Congo
Wanajeshi wa serikali ya DRC wakipigana na waasi wa M23 karibu na Matebe, Kivu, mashariki mwa Congo

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kwamba haitafanya mazungumzo na kundi la waasi la M23, ikilitaja kundi hilo ni la kigaidi.

Katika kikao na waandishi wa habari Jumatatu usiku, msemaji wa serikali ya DRC Patrick Muyaya, amesema kwamba “ni lazima kundi hilo la waasi likabiliwe kwa nguvu za kijeshi ili kurejesha utulivu na amani mashariki mwa Congo.”

“Tunalazimishwa kufanya mazungumzo na makundi ya kigaidi, hilo halitafanyika,” amesema Patrick Muyaya.

Msimamo wa serikali unatofautiana na msimamo wa Umoja wa Afrika, ambao unaitaka serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kufanya mazungumzo na makundi ya waasi yanayopigana mashariki mwa Congo.

Viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki, katika kikao cha Nairobi, walikubaliana kwamba makundi ya waasi yanayopigana mashariki mwa Congo yaweke silaha chini na kundi la M23 liondoke katika mji wa Bunagana.

Msemaji wa kundi la M23 Meja Willy Ngoma, hata hivyo aliiambia Sauti ya Amerika wiki iliyopita kwamba hawataondoka Bunagana na wataendelea kupigana.

Kulingana na mwandishi wetu wa Kinshasa, Serikali ya DRC imesema kwamba itaendelea kulishambulia kundi la waasi la M23 hadi litakapoondoka sehemu hiyo, pamoja na kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu ambao wamekoseshwa makazi.

Serikali ya DRC inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Rwanda imekuwa ikikanusha.

Rwanda badala yake inadai kwamba kundi la waasi la FDLR, linashirikiana na jeshi la DRC kupanga mashambulizi dhidi ya serikali ya Rwanda, madai ambao DRC nayo imekanusha.

Uhasama kati ya DRC na Rwanda umeongezeka

Waandamanaji mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo waliotembea hadi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda wakidai kwamba Rwanda na Uganda zinawaunga mkono waasi wa M23. walibeba mabango yenye picha ya rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni, pamoja na jeneza. Oct 31 2022
Waandamanaji mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo waliotembea hadi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda wakidai kwamba Rwanda na Uganda zinawaunga mkono waasi wa M23. walibeba mabango yenye picha ya rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni, pamoja na jeneza. Oct 31 2022

Hali ya wasiwasi kati ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Rwanda imeongezeka katika siku za hivi karibuni.

Maelfu ya raia wa DRC walifanya maandamano mjini Goma na kutembea hadi kwenye mpaka wa DRC na Rwanda, wakitishia kuvuka mpaka na kuingia Rwanda kabla ya kutawanywa na polisi wa DRC.

Waandamanaji wamekasirishwa na kile wanaamini kwamba “serikali ya Rwanda inaunga mkono waasi wa M23’.

Serikali ya Rwanda imesema kwamba wapiganaji wa FDLR, ambao wanashutumiwa kwa kutekeleza mauaji ya kimbari yam waka 1994, wanashirikiana na jeshi la Congo katika kushambulia waasi wa M23, na kwamba wanaeneza ujumbe wa chuki dhidi ya watu wanaozungumza Kinyarwanda katika Kivu kaskazini.

Msemaji wa serikali ya DRC Patrick Muyaya, ameatoa wito kwa raia wa DRC “kujizuia kueneza ujumbe wa chuki, kufanya ghasia ama kuwashambulia watu wanaozungumza Kinyarwanda mashariki mwa DRC, ili Rwanda isipate sababu ya kutatiza usalama wa DRC”.

Rwanda imeshauri raia wake kutosafiri DRC

Naibu wa msemaji wa serikali ya Rwanda Alain Mukurarinda, ametoa wito kwa raia wa Rwanda kutosafiri DRC kwa ajili ya usalama wao.

Waandamanaji wa mjini Goma vile vile wametaka Uganda kukoma kujiingiza katika maswala ya DRC, wakidai kwamba serikali ya rais Yoweri Museveni nayo inawaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo Patrick Muyaya amesema kwamba “yatachunguzwa na Kinshasa”.

Mapigano yanaendelea Kivu kaskazini kati ya M23 na wanajeshi wa serikali ya Kinshasa.

Kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa – MONUSCO – kimesema kwamba wanajeshi 15 wa DRC wamejeruhiwa katika mapigano hayo, Kiwanja, Rutshuru, na wanatibiwa mjini Goma.

Wanajeshi wa Monusco, wanatoa msaada wa ujasusi kwa jeshi la DRC.

XS
SM
MD
LG