Kiongozi wa chama cha FDC Dkt. Kiiza Besigye alichukuliwa na Polisi wa Uganda Jumatatu alipokuwa akitoka nyumbani kwake akitaka kuelekea kwenye tume ya uchaguzi ili kuhakiki hati zilizosainiwa na mwenyekiti wa tume hiyo kumtangaza Yoweri Museveni kuwa mshindi wa kiti cha rais.
Besigye alionekana mtulivu na hakusema lolote wakati alipokuwa anavutwa na kuingizwa kwenye gari la polisi hata juhudi za waandishi wa habari kumuuliza maswali hazikuzaa matunda.
Polisi walijaribu kuwazuia waandishi wa habari kupiga picha na kuchukua video wakati wa kukamatwa kwake, polisi wakitumia maji yenye pilipili kuwanyunyuzia waandishi wa habari machoni.
Na baada ya kuchukuliwa waandishi wa habari waliwageukia polisi, wakitaka kujua sababu gani polisi hao walitumia pilipili kuwazuia kufanya kazi yao.
Mwandishi wa AFP Isaack Kasamani alipuliziwa pili pili kwenye macho na polisi wa Uganda wakati akijaribu kupiga picha tukio la kumkamata Besigye.
Ilibidi polisi huyo kutoweka, kwani waandishi walitaka kumpiga.
Polisi hao walifunga bara bara na kumpeleka Dkt. Besigye kusikotajwa lakini kwa ushirikiano wa waandishi waliweza kujua kwa kufuata polisi mahala alikopelekwa Besigye katika kituo cha Naggalama, kiasi cha kilometa 50 nje ya jiji la Kampala.
Wakati huo huo ofisi za chama chake cha FDC zilivamiwa na polisi na kukaguliwa, inaaminika kwamba polisi hao wanatafuta ushahidi alio nao Dkt. Kizza Besigye kwamba wizi wa kura ulifanyika kumnyima ushindi katika uchaguzi mkuu uliopita.
Meja Generali Mugisha Muntu kiongozi wa chama cha FDC alizuiliwa kuingia ofisini lakini kulingana na Muntu anasema polisi wanamaliza muda wao kukagua ofisi hizo za FDC na hawatapata chochote.
Polisi pia walizingira tume ya uchaguzi na kumzuia mtu yeyote kuingia au kutoka ndani ya ofisi hizo.
Msemaji wa polisi Fred Enanga naye amesema polisi wana ushahidi kwamba kuna watu wanazisaidia serikali zenye nguvu kubwa duniani kwa kuwapa taarifa ili kuiangusha serikali yake Museveni, pamoja na kumfadhili Besigye.