Timu kadhaa zimeshuhudia kukosa wachezaji wake maarufu kucheza katika mechi muhimu au kukosa kushiriki michuano hiyo moja kwa moja.
Timu ya Gabon Panthers iliwakosa wachezaji wake mashuhuri Pierre Aubomayeng na Mario Lemina ambao baada ya kupona Covid 19 wakagundulika wana matatizo ya moyo.
Timu ya Comoro ilicheza kishujaa bila makipa wake watatu na wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza dhidi ya timu ya Cameroon kwa sababu ya maambukizi ya covid.
Tatizo kama hilo pia lilipiga hodi katika kambi ya timu ya taifa ya Tunisia kabla ya mechi yake na Nigeria.
Maandalizi ya Tunisia kwa mechi yao ya mwisho ya kundi la Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Gambia yalivurugika baada ya wachezaji 12 katika kikosi cha wachezaji 28 kuambukizwa Covid-19, shirikisho la soka la nchi hiyo lilisema.
Nayo Timu ya Burkinafaso ilikosa wachezaji watano muhimu pamoja na kocha wao mkuu Kamou Malo, walipokutwa na virusi wakati wa mechi yao ya ufunguzi dhidi ya Cameroon.
Mchambuzi Ruth Arege kutoka Kenya anasema “wahusika waandaaji wa Afcon wangewapa majukumu kila timu kufanya majaribio yao ili kuwe na uwazi anasema inaonyesha kuna timu zinapendelewa na kuna timu zinaonewa akitoa mfano wa mechi ya Cameroon na Comoro akisema wameona karibu timu nzima ya Comoro kuwa wana covid lakini hilo halijawahi kusikika katika timu ya taifa ya Cameroon.” Aliongeza.
Timu nyingine zilikutana na changamoto hii katika michuano ya awali ya kutafuta nafasi ya kucheza Afcon na kukosa wachezaji wake mashuhuri hasa katika mechi za ugenini wakiambiwa kuwa wamekutwa na covid 19. Mathalan timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars ilipokuwa Antananarivo ilivamiwa na jeshi kwa madai kuwa baadhi ya wachezaji wao wana maambukizi ya virusi vya Corona.
Shirikisho la Soka Tanzania -TFF lilithibitisha timu yao kuwekwa chini ya ulinzi mkali saa chache kabla ya kupambana na Madagascar katika mchezo wao wa mwisho wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia Novemba 2021.
Saleh Ali Jembe ni mchambuzi na mhariri wa Global Publishers anasema “kuna mambo mawili matatu yanajitokeza kuanzia mechi za mtoano za World cup na Afcon unaona kabisa kuna matatizo kwa timu wenyeji kutumia kama fimbo kwa timu wageni wale wachezaji wanaotegemewa zaidi ndio wanatajwa kuwa na Covid, katika michuano hii Burkinafaso walilalamikia wachezaji wao watano katika mechi yao na Cameroon.
Na katika mechi na Comoro makipa wawili mashuhuri walitajwa kuwa na covid kwa hiyo unajiuliza taifa kubwa kama Cameroon vipi inajificha kwenye kivuli cha Covid? Na bahati mbaya zaidi ni vigumu kusema na kujua katika masuala ya kitabibu kujua kama wanaonewa au la, kwa hiyo barani Afrika suala la covid limetumika vibaya na limekuwa kama nyenzo ya kufanya watu wengine washinde mechi badala ya kuwa janga kweli.
Lakini timu kama Comoro zilipeleka malalamiko Shirikisho la soka Afrika -CAF na FIFA lakini yumkini iliwabidi kuendelea na mechi na kulazimika kumweka mchezaji wa ndani kuchukua nafasi ya Golikipa.
Samwel Etoo ndio mwenyekiti wa shirikisho la soka Cameroon na saleh anasema amesikitishwa na Etoo kwani alitarajia kuona vitu vya kimpira zaidi lakini sio vitu vya kiujanja ujanja au sio kwa uoga wa kiasi hiki.