Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:10

COVID -19 : Hali ya maambukizi ilivyoathiri familia nyingi duniani


Magari yakiwa yamejipanga katika uwanja wa mpira Dodger wakazi zoezi la kupima COVID-19 likianza tena baada ya sikukuu ya Krismas huku wimbi jipya la maambukizi likirikodiwa Los Angeles, California, U.S. Disember 29, 2020.
Magari yakiwa yamejipanga katika uwanja wa mpira Dodger wakazi zoezi la kupima COVID-19 likianza tena baada ya sikukuu ya Krismas huku wimbi jipya la maambukizi likirikodiwa Los Angeles, California, U.S. Disember 29, 2020.

Mwaka huu wa 2020 umeshuhudia kila bara kukumbwa na janga la Corona , karibu kila nyumba imeguswa kwa namna moja au nyingine na ugonjwa wa COVID-19.

Janga limeonesha pia jinsi mataifa yalivyo dhaifu katika upande wa huduma za afya.

Takribani mwaka mmoja sasa ulimwengu bado unaendelea kukabiliana na janga la virusi vya Corona ambalo kiini chake kilianzia kwenye jimbo la Wuhan nchini China.

Kwa sasa dunia inazungumzia watu zaidi ya milioni 80 waliokwisha ambukizwa na kupata ugonjwa wa COVID-19, na vifo vya watu zaidi ya milioni moja na laki saba, kulingana na chuo kikuu cha John Hopkins cha Marekani katika kitengo kinachofuatilia kesi za virusi vya Corona.

Marekani inaongoza Duniani ikiwa na zaidi ya watu milioni 18 waliopatwa na COVID, na vifo zaidi ya laki tatu.

Kwa mujibu wa shirika la Habari la Reuters, bara la Afrika lina kesi takribani milioni mbili na nusu, huku Afrika kusini ikiwa inaongoza. Ushirikiano wa utafiti kati ya wanasayansi kutoka mataifa mbali mbali Duniani, umesaidia hatimaye kupatikana kwa chanjo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Rais mteule wa Marekani Joe Biden akipatiwa chanjo ya COVID-19
Rais mteule wa Marekani Joe Biden akipatiwa chanjo ya COVID-19

Barani Afrika, nchi ya Kenya na Afrika Kusini ni mojawapo ya nchi zilizohusika kufanya utafiti, huku Kenya ikifanya hivyo kupitia taasisi ya utafiti wa tiba ya KEMRI, pamoja na chuo kikuu cha OXFORD cha London, kwa kushirikiana na kampuni ya kutengeneza dawa ya AstraZeneca.

Wanasayansi wa Marekani walikua wa kwanza kutangaza wamefanikiwa kupata chanjo ya Corona, iliyotengenezwa na kampuni za Pfizer na BioNTech ya Ujerumani, ikifuatiwa na kampuni ya Moderna na kuidhinishwa na serikali kuu ya Marekani, na kuanza kutolewa siku kadhaa zilizopita kwa wazee, na kundi la kwanza la wafanyakazi wa huduma ya afya.

Huko Uingereza, Margaret Keenan, alipokea zawadi bora katika siku yake ya kuzaliwa akifurahia miaka 91. Aliweka historia kama mwanamke wa kwanza kupatiwa chanjo ya COVID huko Uingereza.

Chanjo ya Pfizer-BioNtech ya Covid-19
Chanjo ya Pfizer-BioNtech ya Covid-19

Keenan anaeleza : "Kwa sasa sijui ninajisikiaje. Ni kitu cha ajabu na cha kufurahia sana kwa kweli. Ndio hivyo, hii ni kwa sababu nzuri, kwa hivyo nimefurahishwa kuchukua hatua hiyo//End Act//

Wakati chanjo ya COVID inatarajiwa pia kufika Afrika mapema mwakani, naye mkurugenzi wa taasisi ya kuzuia na kudhibiti magonjwa barani Afrika-Africa CDC, John Nkengasong, anasema Afrika inalenga kutoa chanjo hadi asilimia 60 ya watu wake bilioni 1.3 katika kipindi cha miaka miwili ijayo, lakini inaweza kuhitajika miaka kadhaa ya utoaji chanjo.

Anasema haijulikani bado ni mara ngapi watu watahitajika kupatiwa chanjo dhidi ya COVID. Na kwa sababu hiyo utengenezaji wa ndani kwa chanjo ya COVID-19 ni muhimu, ili kuweza kufikia malengo kwa jamii.

Hata hivyo afisa wa juu wa WHO Mike Ryan, anasema pamoja na mafanikio haya, lakini ni lazima kuchukua tahadhari zaidi.

Ryan anafafanua : "Ningependa kusema chanjo hazilingani katika kutokomeza COVID. Chanjo na uchomaji chanjo utaongeza hatua moja kubwa sana kwenye vifaa ambavyo tunavyo. Lakini peke yao, hawataweza kufanya kazi hiyo. Na kwa hivyo inatubidi tuongeze chanjo katika mkakati uliopo, wa afya ya umma.

Makamu wa Rais Mike Pence akipatiwa chanjo ya COVID-19
Makamu wa Rais Mike Pence akipatiwa chanjo ya COVID-19

Ugonjwa mwingine ambao umetikisa jamii katika kanda ya Afrika mashariki hususan Kenya ni saratani. Huu ni ugonjwa wa tatu unaosababisha vifo vingi nchini Kenya, kulingana na shirika la afya Duniani-WHO, na idadi inaongezeka kutoka wagonjwa takribani 37,000 walioripotiwa mwaka 2012 hadi zaidi ya watu 48,000 hivi sasa.

Dr.Gladwell Kiarie, ni mtaalamu wa saratani katika hospitali ya Nairobi. Anahamasisha kuwepo na ongezeko la uchunguzi wa saratani, na pia kuwepo mabadiliko ya mfumo wa maisha.

Kiarie anaeleza :"Tunavuta sana sigara. Tunakunywa sana pombe. Ulaji wa vyakula vyetu vya asili umebadilika, na hatuli vyakula hivyo kama tulivyozoea. Tunakula vyakula vingi vyenye mafuta. Hatunywi maji mengi wala mboga za majani, tunakula zaidi vyakula kutoka viwandani, ambavyo tayari vimeshaandaliwa.

Serikali ya Kenya imeonesha mwamko kwa kufanya kampeni zinazotoa ufahamu juu ya tatizo hili, pamoja na kufungua vituo vingi vinavyopima saratani takribani nchi nzima. Lakini wakenya wengi wanaoishi chini ya dola tatu kwa siku, hawawezi kumudu gharama za matibabu.

Hata hivyo janga la Corona limevuruga mpangilio wa matibabu na huduma nyingine muhimu zinazohusiana na tiba ya saratani.

Na takribani miaka 40 tangu kugundulika kwa ukimwi. HIV bado ni changamoto kuu ya afya ya umma, na janga la COVID-19 limeongezea hali kua ngumu kupata matibabu kwa jamii.

Hata hivyo UNITAID, WHO na wadau wengine wa afya walitangaza mwaka huu, kupatikana kwa dawa ya kupunguza makali ya virusi vya ukimwi yenye ladha tamu ya matunda ya STRAWBERRY, kwa ajili ya Watoto. Umoja wa Mataifa unakadiria watoto takribani milioni 1.7 kote duniani wanaishi na virusi hivyo, lakini ni nusu pekee ya idadi hiyo ndio wanaopokea matibabu.

Moja ya kile inachofanya hali kuwa ngumu kwa watoto wadogo kunywa dawa hizo, ni ladha yake chungu. Na pia gharama ya juu licha ya hatua kubwa kufanyika katika miaka ya karibuni. Dawa hizo zitaanza kutolewa miaka michache ijayo nchini Kenya, Malawi, Zimbabwe, Nigeria na Benin.

Wakati huo huo baraza la kitaifa la kudhibiti ukimwi Kenya-NACC, linaeleza kuna ongezeko la kesi za maambukizi mapya ya ukimwi kwa Watoto na vijana. Mwaka huu pekee wanafunzi zaidi ya 21,400 wameambukiza wengi wakiwa wasichana na baadhi wavulana, wote wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 19. Miongoni mwa kile kilichochangia ni watoto kulazimika kukaa nyumbani tangu Machi wakati shule zilipofungwa, ili kuzuia kusambaa kwa janga la COVID-19.

Ili kukabiliana na changamoto ya maambukizi mapya ya HIV, shirika moja kutoka Ujerumani la DSW linaendeleza kampeni ya kujengwa kwa vituo vya afya vinavyotoa elimu juu ya ukimwi, ambavyo wahudumu wake ni vijana. Huyu hapa Abdalla Saha, mtoa ushauri kituo cha afya cha Rabai.

Saha anasema :"so watu huwa wanakuja hapa tunawapokelea hapa,,,,pia wanajisikia.

Lakini pia vijana wamepokea vipi kuwepo kwa vituo hivi ambavyo wanaviona kama rafiki kwao, licha ya kuwa wanapata elimu juu ya kutunza afya zao. Anaeleza mmoja wa vijana hao Paulin kutoka pwani ya Kenya.

Pauline anaeleza : "Hii center kuna watu (wanaushirikiano zaidi) "more friendly" ni vizuri zaidi kuwaelezea kile ninahitaji compare na kwenda hospitali//End Act//

Kwa sababu ya kuenea kwa ugonjwa wa COVID-19, sekta ya huduma ya afya imekuwa gumzo kwa mwaka wote wa 2020. Pamoja na mabadiliko makubwa namna kazi inavyofanyika, sekta ya huduma ya afya imelazimika kuanzisha kanuni na miongozo mipya kwa wagonjwa.

Mahitaji ya huduma hospitalini kwa wagonjwa wa COVID-19, imefanya iwe vigumu kwa watu wengine wenye matatizo sugu ya kiafya kupata matibabu kwa wakati. Wengi pia wameepuka kutembelea hospitali kwa kuhofia kuambukizwa virusi. Ili kuziba pengo hili kati ya wagonjwa na daktari, ndipo ilipoanzishwa huduma ya Telemedicine, ambapo mtu hahitajiki kukutana ana kwa ana na daktari, badala yake kuwasiliana na daktari kupitia mtandao.

Huduma za afya kwa njia ya digitali, pia zilikuwepo hapo awali lakini ziliongeza umaarufu 2020, kwa kuwa wagonjwa wengi Duniani walihitaji ustadi wa kudhibiti hali zao za kiafya za muda mrefu, wakati wanapokuwa nyumbani. Anaeleza ofisa mkuu wa habari katika Permanente Federation

Dr. Edward Lee anasema :"Kuangalia sehemu yenye upele, sehemu yenye madoa mkononi, hilo ni jambo zuri katika afya kwa njia ya mtandao, kwa sababu tuna uwezo wa kuona kupitia video. Kushika sehemu yenye uvimbe na kuangalia kama ni ngumu au la, hilo ni jambo gumu kidogo japokuwa tunaweza kumuuliza mgonjwa aelezee mwenyewe jinsi anavyohisi ili kuweza kufahamu.

Lakini Dr Lee anasema kama anahitaji kumchoma sindano mgonjwa, hawezi kufanya hivyo kwa njia ya video au simu. Inapofika hatua ya namna hiyo, mgonjwa anahitajika kuonana uso kwa uso na daktari, pamoja na kufika hospitalini.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Mkamiti Kibayasi, Washington DC

XS
SM
MD
LG