Maambukizi ya kila siku yanasemekana kupanda hadi zaidi ya 26,900 hapo Jumatano na 24,700 Alhamisi ikiwa kiwango cha juu zaidi tangu kutokea kwa aina mpya ya virusi vya omicron.
Viwango sawa na hivyo vinasemekana kushuhudiwa Juni na Julai wakati wa maambukizi ya virusi vya delta. Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, wataalam wameongeza kusema kwamba licha ya ongezeko la maambukizi, idadi ya vifo bado haijapanda na kwamba hilo huenda likashuhudiwa baada ya muda wa wiki kadhaa.
Asilimia 90 ya maambukizi mapya yanasemekana ni kutokana na aina mpya ya virusi vya omicron kulingana na vipimo vya kila siku. Sasa hivi maambukizi yanasemekana kuenea kwenye majimbo yote 9 ya Afrika kusini baada ya kushuhudiwa mwanzoni kwenye jimbo la Gauteng ambako iko miji ya Johannesburg na Pretoria.