Chombo cha utafiti cha idara ya mambo ya anga ya Marekani NASA kinachojulikana kama Juno kimetuma picha yake ya kwanza ya sayari ya Jupiter toka kilipowasili katika sayari hiyo.
Idara hiyo ya Marekani imetoa picha inayoionyesha sayari ya Jupiter ikiwa imezungukwa na miezi yake minne mikubwa.
Juno ilifika katika mzunguko wa Jupiter wiki iliyopita baada ya safari yake ya miaka mitano, ya kusafiri kilometa bilioni 2.8.
Waendeshaji wa chombo hicho waliopo duniani walizima kamera na vyombo vingine vya chombo hicho kilipokuwa kunapita mazingira ya Jupiter yenye mionzi mikali.
Kamera ya Juno inatarajiwa kutuma picha zenye ubora wa juu za Jupiter mwezi ujao wakati kitakapo safari kuisogelea zaidi sayari hiyo.