China Jumanne iliahidi dola milioni 230 kuanzisha mfuko wa kulinda viumbe na mimea katika mazingira Biodiversity katika nchi zinazoendelea. Rais Xi Jinping akizungumza kwa njia ya video kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa katika mji wa Kunming, kusini magharibi mwa China, alitoa wito kwa nchi zingine kuchangia mfuko wa Biodiversity.
Mkutano wa wiki nzima unaashiria kuanza rasmi kwa duru mpya wa mazungumzo juu ya kulinda mimea na wanyama kutotoweka. Kikao cha pili na cha mwisho ambacho kitajaribu kukubaliana juu ya malengo kwa miaka 10 ijayo kimepangwa kufanyika Kunming kutoka April 25 hadi Mei 8 mwaka ujao.
Dunia imeshindwa kufikia malengo mengi ya sasa ya miaka 10 malengo ya Aichi Biodiversity yaliyowekwa Japan mwaka 2010. Greenpeace, kikundi cha mazingira kimesema nchi zinahitaji kuzingatia sio tu kuweka malengo mapya lakini pia kuyatimiza.