Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 24, 2024 Local time: 16:07

Charles Njonjo, Mwanasheria mkuu wa Kwanza wa Kenya huru, afariki


Charles Mugane Njonjo, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Kenya aliyeaga dunia Jumapili tarehe 2 mwazi Januari, 2022.
Charles Mugane Njonjo, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Kenya aliyeaga dunia Jumapili tarehe 2 mwazi Januari, 2022.

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa kwanza wa Kenya baada ya uhuru wa nchi hiyo, Charles Mugane Njonjo, aliaga dunia Jumapili tarehe 2 Januari 2022, akiwa na umri wa miaka 101.

Akitangaza kuhusu kifo chake, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema Njonjo, aliyefahamika na Wakenya wengi kama Sir Charles, alikuwa mmoja wa watu waliokuwa na mchango mkubwa katika historia ya taifa hilo la Afrika Mashariki.

Familia ya Njonjo ilitanmgaza kwamba kifo chake kilisababishwa na homa ya mapafu.

“Kifo cha Mheshimiwa Njonjo siyo pigo tu kwa familia yake, marafiki na jamaa zake, bali ni pigo kwa Wakenya wote, Bara la Afrika kwa sababu ya juhudi zake za kujenga msingi wa kupatikana uhuru wa Wakenya,” Kenyatta alisema.

Alisema Kenya ina kila sababu ya kujivunia kazi nzuri ya Njonjo na viongozi wote waliokuwa katika mstari wa mbele kupigania uhuru kwa kujinyima ili kutengeneza mazingira mazuri kwa vizazi vya wakati huo na vya baadaye, na kuongeza kwamba Kenya inamshukuru Njonjo na viongozi wa kizazi chake kwa kuweka msingi wa siasa za nchi.

“Ama kwa hakika ni Mheshimiwa Njonjo na kizazi cha viongozi wa enzi ya uhuru walioweka msingi ambao taifa letu linatumia kustawi,” alisema.

Njonjo alihudumu katika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 1979.

Vilevile alikuwa Waziri wa Masuala ya Kikatiba kuanzia mwaka 1980 hadi 1983.

Alliingia bungeni mnamo 1980 baada ya kustaafu kama Mwanasheria Mkuu akiwa na umri wa miaka 60.

Alichaguliwa bila kupingwa kama Mbunge wa eneo wakilishi la Kikuyu, baada ya mbunge aliyekuwepo kujiuzulu siku ambapo Njonjo alitangaza nia yake ya kuwania kiti hicho.

Ni wakati huo ambapo Rais wa pili, Hayati Daniel Moi alimteua Njonjo kushikilia wadhifa wa Waziri wa Masuala ya Kikatiba. Alihudumu katika cheo hicho kuanzia 1980 hadi 1983 alipopigwa kalamu kwa tuhuma za kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali mnamo Agosti 1, 1982.

Njonjo ni mjumbe pekee katika baraza la kwanza la mawaziri lililoundwa na Rais wa kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta mwaka 1963, ambaye mpaka sasa alikuwa hai.

Mwili wa Njonjo ulichomwa saa chache baada ya kifo chake, kwa kuzingatia azma yake alipokuwa hai.

Amemuacha mjane, Margaret Bryson, na watoto watatu.

XS
SM
MD
LG