Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:40

Changamoto zinazo ikabili Mahakama Maalum Uganda


Imetimia miaka 10 tangu Uganda ilipoanzisha mahakama ya kusikiliza kesi za uhalifu wa kimataifa zinazohusu vita, dhulma na mauaji ya halaiki, yanayodaiwa kutekelezwa nchini Uganda katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.

Ufanisi wa mahakama hiyo hata hivyo unatiliwa shaka, baada ya kukosa kusikiliza na kuamua kesi maarufu nchini humo zinazohusu uhalifu dhidi ya binadamu.

Idara ya mahakama ya kusikiliza kesi za uhalifu wa kimataifa nchini Uganda, iliundwa baada ya mazungumzo ya Amani yaliyomaliza vita vya miaka 20 kati ya serikali na waasi wa Lords Resistance Army –LRA- wakiongozwa na Joseph Kony.

Joseph Kony

Mahakama hiyo iliundwa ili kufanya kazi kwa karibu na mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kibinadamu ya ICC, yenye makao yake makuu mjini Hague, Uholanzi, baada ya ICC kutoa kibali cha kutaka kamanda wa LRA Joseph Kony akamatwe na kufikishwa mbele yake.

Laking tangu kufunguliwa kwake, mahakama hiyo ya Uganda mpaka sasa imewahukumu watu sita kwa makosa ya ugaidi. Washukiwa wote walihusishwa na makosa ya kuwauwa viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Uganda.

Thomas Kwoyelo

Kesi nyingine iliyoko katika mahakama hiyo ina mhusisha mmoja wa makamanda wa LRS, Thomas Kwoyelo aliyekamatwa nchini Congo, miaka tisa iliyopita. Kesi hiyo inaanza mwezi June.

Msajili wa mahakama hiyo Harriet Ssali amesema kwamba inakabiliwa na changamoto nyingi na hususan idadi kubwa ya kesi zilizorudikana.

“Mahakama hii inashughulikia maelfu ya kesi kwa niaba ya raia wote wa Uganda. Huwezi ukasema kwamba nimemfungulia Kwoyelo mashtaka kwa sababu ya makosa ya vita aliyofanya na kwamba nisishughulikie Zaidi ya kesi 10,000 zinazohusu ngono na watoto, mauaji, unajisi na kadhalika. Uganda nzima inahitaji haki,” ameeleza Ssali.

Jamil Mukulu

Kwa sasa, mahakama hiyo inaendesha kikao kutafuta jinsi kesi ya aliyekuwa kamanda wa kundi la waasi la Allied Democratic Forces – ADF- Jamil Mukulu itakavyosikilizwa, ambacho kimechukua mapumziko ya wiki mbili ili kudurusu ushahidi uliotolewa na serikali ya Tanzania.

Mahakama yakosa Wataalam

Mtaalam wa Sheria Wandera Ogaalo, anasema kwamba mahakama hiyo ina mapungufu makubwa katika idhara yake ya upelelezi.

Mtaalam huyo amesema:"Hatuna wataalam wa upelelezi katika Nyanja hii. Waliopo wanashughulikia kesi za uhalifu wa kimataifa, jinsi wanavyoshughulikia kesi za kawaida. Zingatia kwamba hizi ni kesi za mauaji ya halaiki ya watu na dhulma dhidi ya binadamu. Haya ni makosa ambayo hayapo katika sheria zetu. Sasa, utawezaje kutegemea maafisa wetu wa polisi wasio na tajriba ya kutosha kuchunguza kesi hizi?”

Sheria ya mwaka 2000

Changamoto nyingine inayotajwa kama kizingiti kwa mahakama ya uhalifu nchini Uganda ni sheria ya mwaka 2000 inayotoa msamaha kwa wapiganaji, iliyotungwa ili kuwahimiza wapiganaji kuacha vita na ahadi ya kusamehewa.

Kweyelo, alijaribu kuomba msamaha ili kuepuka kufikishwa mahakamani lakini ombi lake lilikataliwa na mahakama ya kilele mnamo mwaka 2015.

Baadhi ya wanachama wa kundi la waasi la ADF wanaokabiliwa na mashtaka mahakamani wanadai kwamba maafisa wa serikali wamewahimiza kuomba msamaha.

Utaratibu wa misamaha

Ssali anasema kwamba mahakama ya uhalifu wa kimataifa, inakubali washukiwa kusamehewa lakini tendo la kutolewa msamaha lazima lifuate mwelekeo uliopo na wanaoomba msamaha lazima wawe wale waliojisalimisha na kuacha vita.

Ssali anafafanua kuwa: "Sheria ya kwanza kuhusu msamaha ilikuwa na makosa. Ilikuwa inatoa msamaha bila kuzingatia masharti bila kuweka bayana mazingira ambayo unaweza kuomba msamaha. Watu walifuarahia kwa sababu walitaka kumaliza vita kaskazini mwa Uganda. Walitumia sharia hiyo kama kichocheo cha kumaliza vita kw akuahidi msamaha kwa kila aliyekuwa akiendeleza vita lakini hilo haliwezi kutumika kwa kila mtu.”

Wabunge wanazingatia kuifanyia marekebisho sheria ya kutoa msamaha ili kuweka bayana orodha ya watu wanaostahili kusamehewa, na masharti ya kupata msamaha huo.

XS
SM
MD
LG