Bila kutoa Ushahidi wowote, msemaji wa chama cha ZANU-PF Patrick Chinamasa ameambia waandishi wa habari kwamba balozi wa Marekani mjini Harare Brian Nichols, anajihusisha na vitendo vya kutaka kuinagusha serikali ya rais Emmerson Mnangagwa.
Madai ya Chinamasa yanafanana na aliyokuwa akitoa aliyekuwa rais wa nchi hiyo marehemu Robert Mugabe.
Serikali ya Zimbabwe ilikuwa ikishutumu Marekani na Uingereza kila mara kwamba zilikuwa na lengo la kuipindua serikali ya aliyekuwa rais Mugabe.
ZANU-PF kimedai kwamba balozi Nicholas, anaendelea kujihusisha na mambo yanayoidharau serikali kwa kufadhili makundi yanayopinga serikali na kutoa mafunzo kwa wapiganaji, kikiongezea kwamba serikali haitachelewa kumfukuza nchini humo endapo hatabadilisha mwenendo wake.
Msemaji wa chama hicho amesema kwamba mabalozi hawastahili kuwa na tabia kama za majambazi, na kwamba balozi Nicholas ni jambazi.
Ubalozi wa Marekani mjini Harare haujajibu madai hayo.
Hali ya wasiwasi inaendelea kuongezeka nchini Zimbabwe baada ya wanaharakati kuitisha maandamano Julai 31 kupinga ufisadi serikalini, na hali mbaya ya uchumi unaoendelea kuharibika zaidi.
Mwezi uliopita, serikali ya Zimbabwe ilimuita balozi Nichols baada ya afisa wa ngazi ya juu wa White House kusema kwamba Zimbawe ilikuwa miongoni mwa nchi zilizokuwa zikichochea maandamano ya nchini Marekani, kufuatia kifo cha George Floyd.
Balozi za Marekani, Uingereza, umoja wa ulaya na ofisi ya umoja wa mataifa, zimeoikosoa Zimbabwe kwa kuwakamata waandishi wa habari na wapinzani wa kisiasa.
Uhusiano kati ya Zimbabwe na mataifa ya magharibi ulikuwa umeanza kuonyesha dalili za kuboreka chini ya utawala wa Rais Emmerson Mnangagwa, lakini tena umeingia doa kufuatia rekodi mbaya ya haki za kibinadamu.
Msemaji wa chama kinachotawala cha ZANU-PF, amehimiza wafuasi wake kujilinda dhidi ya waandamanaji na kujizuia na ghasia kama zilizotokea kati ya Agosti 2018 na Januari 2019 baada ya uchaguzi mkuu, kupinga bei ya juu ya Mafuta.
Waandalizi wa maandamano wamesema kwamba maandamano yao ya wiki hii yatakuwa ya amani lakini Chinamasa amewataka wafuasi wa ZANU-PF kutumia kila mbinu kujilinda.
-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC