Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Januari 05, 2025 Local time: 10:07

Chama kipya chaundwa Tanzania kuendeleza falsafa ya Magufuli


Aliyekuwa rais wa Tanzania hayati John Magufuli (Kulia) na rais wa sasa wakati huo akiwa makam wa rais Samia Haasan Suluhu (kushoto) March 17,2021. PICHA: AFP
Aliyekuwa rais wa Tanzania hayati John Magufuli (Kulia) na rais wa sasa wakati huo akiwa makam wa rais Samia Haasan Suluhu (kushoto) March 17,2021. PICHA: AFP

Chama kipya cha kisiasa kimeanzishwa nchini Tanzania, kikiwa na lengo la kuendeleza sera na mtindo wa uongozi wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli.

Waanzilishi wa Umoja party wanaripotiwa kuwa wanachama na watu maarufu ndani ya chama kinachotawala cha CCM, ambao hawana furaha na uongozi wa sasa.

Mwanzilishi wa chama hicho Seif Maalim Seif, ameambia sauti ya Amerika VOA kwamba “Tuliwasilisha maombi ya usajili mwaka jana na tumefikia hatua ya marekebisho kadha wa kadha. Katika Ofisi ya msajili wa vyama kuna katiba na kanuni za chama chetu na vielezo vyote vinavyotakiwa.”

Baadhi ya vigogo wa CCM wanaunda Umoja party?

Kuna ripoti kwamba huenda watu maarufu na wa ngazi ya juu katika chama kinachotawala, ambao wangependelea Tanzania iongozwe namna alivyokuwa anaongoza aliyekuwa rais wa nchi hiyo hayatoi John Pombe Magufuli, ndio wanaosukuma kuundwa kwa chama cha umoja.

“Chama chetu kilifikia hatua ya kuwekwa kwenye gazeti la serikali mwezi Novemba mwaka jana kwa mda wa siku 21 kwa yeyote aliye na pingamizi. Kwa hivyo hiki chama sio kwamba watu wamejikusanya na kuamua kufanya hivi na hivi. Tunachosubiri ni maelekezo ya msajili wa vyama kwa ajili ya kupewa cheti cha usajili.” Amesema Maalim Seif.

Picha za watu ambao wamevalia fulana za chama cha umoja, zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii. Fulana hizo zina picha ya aliyekuwa rais wa Tanzania John Magufuli.

“sisi wa upande wetu hatuna deni lolote la mahitaji ya kisheria ya kutaka kusajiliwa. Ni Afisi tu ya msajili wa vyama kutuambia kiachofuata. Tulishamaliza mwaka mmoja sasa.” Ameongezea Seif Maalim Seif.

Malengo ya umoja party

Misingi ya chama hicho ni kuendeleza falsafa ya aliyekuwa rais John Mgufuli. Waanzilishi wake wanasema kwamba Tanzania sasa ipo katika hali ya sintofahamu, miongoni mwa vyama vya kisiasa huku hali ya maisha kwa watanzania ikiendelea kuwa ngumu, na kwamba ipo haja ya kufuata nyayo za Magufuli kuongoza taifa hilo.

Hata hivyo, Seif Maalim amesita kusema iwapo chama cha mapinduzi kina mapungufu kwa sasa kuendeleza falsafa ya Magufuli akisema kwamba “nadhani falsafa yake, kama chama cha mapinduzi kinaitumia au la, ni jukumu la wananchi wenyewe kuamua.”

Wanachama wengine wa Umoja party hata hivyo bado ni siri ya wenye chama.

“Jamii inaona ukweli ni akina nani wana dhati ya kumuenzi rais Magufuli. Wale ambao wapo tayari kupoteza nyadfa zao, na wale wanaoona kwamba falsafa ya Magufuli haitekelezwi. Siwezi kuwataja majina lakini dhamira zao zinajulikana.” Amesema Maalim Seif, akiongezea kwamba “wimbi la kisiasa ni la kawaida” akiwa anajibu swali iwapo kuundwa kwa umoja Party kutavuruga chama cha CCM ambacho alikipenda John Magufuli.

Mvutano ndani ya chama cha CCM

Mnamo mwezi Januari, mjadala mkali ulitokea Tanzania kuhusu deni la nchi hiyo linaloendelea kuongezeka, baadhi ya viongozi katika chama kinachotawala cha CCM wakisikika hadharani wakimkosoa rais Samia Suluhu Hassan kwa kile walisema ni “kuendelea kukopa kiholela” ili kufadhili miradi ya serikali.

Mjadala huo ulipelekea spika wa buge la taifa Job Ndugai kujiuzulu.

Ndugai alikuwa miongoni mwa viongozi wakuu wa CCM walikosoa uongozi wa rais Samia, ambaye baadaye alifanya mabadiliko serikali na kuwatimua baadhi ya viongozi, siku chache baada ya kusema hadharani kwamba angewatimua wale ambao wanataka kufanya siasa badala ya kutumikia wananchi kuleta maendeleo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG