Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:35

Burundi Yakumbuka Mauaji ya Rais Ndadaye Miaka 27 Baadaye


President Melchior Ndadaye
President Melchior Ndadaye

Burundi imeadhimisha miaka 27 tangu kuuawa kwa rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia nchini humo Melchior Ndadaye.

Ndadaye, Mhutu, aliuawa Oktoba 21 1993, siku 102 baada ya kuapishwa kuwa rais wa Burundi.

Licha ya kuidhinishwa kwa mkataba wa Februari 5 1991 wa makabila yote ya Burundi kuishi kwa umoja na amani hasa makabila ya Hutu, Tutsi na Twa, ghasia zilitokea nchini humo baada ya kuuawa kwa Ndadaye, na kusababisha vifo vya watu 300,000.

Jumatano wiki hii, rais wa sasa wa Burundi Evariste Ndayishimiye, aliongoza taifa hilo kwa maadhimisho rasmi ya miaka 27 tangu kuuawa kwa Ndadaye.

Ofisi ya rais ilisema kwamba mauaji ya Ndadaye “yalipangwa na wahalifu akiwemo mrithi wake, Pierre Buyoya.”

Jumanne wiki hii, mahakama ya juu ya Burundi ilimhukumu aliyekuwa rais Pierre Buyoya na wenzake 18 maisha gerezani bila ya kuwepo mahakamani kwa kile kilitajwa kama “mchango wao katika mauaji ya Ndadaye.”

Watu hao 19 walipatikana na makosa ya kushambulia kiongozi wa nchi na kujaribu kusababisha mauaji ya halaiki ya watu na uharibifu mkubwa nchini Burundi.

Aliyekuwa waziri mkuu Antoine Nduwayo, aliondolewa mashtaka hayo na mahakama, baada ya kukosekana ushahidi dhidi yake kwamba alishiriki katika njama hiyo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG