Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 12:20

Burundi yafungua mipaka yake na Rwanda


Ramani ya Burundi.
Ramani ya Burundi.

Burundi hatimae imefungua upande wake wa mpaka kuingia Rwanda siku ya Ijumaa baada ya kukataa kufanya hivyo mapema mwaka huu pale Rwanda ilipoamua kufungua mipaka na jirani yake.

Rwanda ilifungua mipaka yake mapema mwaka huu baada ya kufungwa kwa zaidi ya miaka miwili kufuatia mvutano wa kisiasa kati ya nchi hizo jirani.

Serikali ya Bujumbura iliendelea kuishtumu Kigali kwa kutowakabidhi kwa vyombo vya sheria vya Burundi watu wanaoshukiwa kushiriki katika njama ya kupindua utawala wa hayati Rais Pierre Nkurunziza tarehe 13 Mei mwaka wa 2015.

Rwanda iliendelea kueleza kwamba haiwezi kuwafurusha au kuwarejesha nchini mwao, watu waliopewa hifadhi chini ya sheria ya kimataifa inayohusu wakimbizi.

Ilikuwa furaha tele kwa wasafiri wanaoelekea Rwanda kutoka Burundi ambao wameingia kwa mara ya kwanza nchini Rwanda tangu mwaka wa 2020 bila kuomba ruhusa maalum kutoka kwa wizara ya mambo ya ndani ya Burundi, kulingana na mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kirundi na Kinyarwanda ya Sauti ya Amerika mjini Kigali.

Ilikuwa pia habari njema kwa wakazi wanaoishi katika mikoa ya Burundi inayopakana na Rwanda, hasa wafanyabiashara wadogo wadogo, ambao wamekuwa wakilakamika kwamba hatua ya kufunga mipaka iliwaathiri sana na kusababisha umaskini katika familia zao.

Viongozi wa Burundi na Rwanda wamesikika mara kadhaa wakisema kwamba wako tayari kufufua tena uhusiano kati ya nchi zao.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na Burundi walikutana zaidi ya mara mbili katika ziara rasmi, hata maafisa wa usalama walikutana mara kadhaa eneo la mpakani kujadili namna ya kuimarisha usalama kati ya nchi hizo mbili.

Wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wanasema mvutano kati ya majirani hao wawili utamalizika kabisa, wakati ma rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye na wa Rwanda Paul Kagame watakapokutana ana kwa ana na kuafikiana kumaliza tofauti kati ya nchi zao.

XS
SM
MD
LG