Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 03, 2025 Local time: 05:46

Bunge la Somalia laidhinisha baraza jipya la mawaziri


Waziri Mkuu wa Somalia, Omar Abdirashid Ali Sharmarke
Waziri Mkuu wa Somalia, Omar Abdirashid Ali Sharmarke

Bunge la Somalia limeidhinisha baraza jipya la mawaziri Jumatatu saa kadhaa baada ya watu wenye silaha kumfyatulia risasi na kumuuwa mbunge mmoja.

Abdullahi Qayad Barre aliuwawa katika eneo la hamar jajab kwenye mji mkuu, Mogadishu. Mbunge mwenzie Mohamed Ali Hagaa alisema Barre alikuwa njiani kuelekea bungeni wakati alipofyatuliwa risasi na kuuwawa ndani ya gari lake kwenye makutano ya barabara yenye harakati nyingi.

Washambuliaji walikimbia kutoka kwenye eneo na kundi la wanamgambo wa al-Shabab lenye uhusiano na al-Qaida lilidai kuhusika na mauaji hayo.

Wabunge wakiwa bungeni Somalia
Wabunge wakiwa bungeni Somalia

Licha ya mauaji hayo kutokea bunge lilikutana na kuidhinisha baraza la mawaziri la Waziri Mkuu, Omar Abdirashid Sharmarke.

Baraza jipya la mawaziri linajumuisha wanachama 66 wengi wao ni wabunge. Hii ilikuwa ni orodha ya pili ya Waziri Mkuu kwa mawaziri hao baada ya orodha ya kwanza kukataliwa.

Wafadhili wa kimataifa wanaonya kwamba mapigano yasiyoisha ya ndani kwa ndani miongoni mwa wanasiasa nchini humo yanadumaza juhudi za kuimarisha nchi hiyo iliyokumbwa na vita.

Kundi la wanamgambo wa al-Shabab limepoteza maeneo yake mengi iliyowahi kuyadhibiti awali lakini kundi hilo linaendelea kuwa kitisho kwa serikali. Wapiganaji wa al-Shabab walifanya mashambulizi makubwa mawili kwenye makazi ya rais mwaka jana na hapo Disemba 25 walishambulia kituo kimoja cha walinda amani wa Umoja wa Afrika ambao wanaisaidia serikali ya Somalia.

XS
SM
MD
LG