Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:38

Botswana yarejesha masharti ya kukaa nyumbani kukabiliana na Corona


Barabara isiyo na shughuli nyingi nchini Botswana. (Mqondisi Dube/VOA)
Barabara isiyo na shughuli nyingi nchini Botswana. (Mqondisi Dube/VOA)

Serikali ya Botswana imefunga tena shughuli za kawaida na kutaka watu wasalie nyumbani kwa mda wa wiki mbili kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona kwa kasi nchini humo.

Wafanyakazi muhimu pekee ndio wanaruhusiwa kuondoka nyumbani kwao na kuelekea kazini huku watu wengine wakiruhusiwa tu kuondoka nyumbani iwapo wanaenda kununua chakula au kutafuta matibabu.

Mikusanyiko ya watu imepigwa marufuku huku hoteli, maeneo ya mazoezi, migahawa na shule, vimefungwa.

Shughuli katika mji mkuu Gaborone zimesitishwa mwezi mmoja na nusu baada ya kufunguliwa. Shule na biashara zilifunguliwa Juni 15 pale maambukizi yaliripotiwa kupungua.

Nchi hiyo yenye utajiri wa almasi, imerekodi kasi kubwa ya maambukizi a virusi vya Corona, kwa mujibu wa msimamizi wa tume maalum ya kupambana na Corona Kereng Masupu, ambaye alisema kwamba “wiki hii tumeona ongezeko la maambukizi kwa kasi, kinyume na ilivyotarajiwa na sasa inatubidi kusitisha tena shughuli za kawaida na kutekeleza mikakati ya kukabiliana na maambukizi.”

Idadi ya watu ambao wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona nchini Botswana imeongezeka mara mbili zaidi kutoka watu 71 July 13 hadi watu 140.

Kufikia Alhamsi, jumla ya watu 800 walikuwa wameambukizwa virusi vya Corona nchini Botswana, watu 664 wakiwa madereva wa magari ya kubeba mizigo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG