Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 12:03

Wataalam wa usalama watia shaka madai ya utekaji nyara Nigeria


Vijana wa shule walioachiwa huru wakiwa kwenye mkutano na rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, Dec. 18, 2020 huko Katsina, Nigeria(AP Photo/Sunday Alamba).
Vijana wa shule walioachiwa huru wakiwa kwenye mkutano na rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, Dec. 18, 2020 huko Katsina, Nigeria(AP Photo/Sunday Alamba).

Wataalam wa usalama wa Nigeria wanatia shaka madai ya maafisa kwamba uhasama kati ya wakulima na wafugaji wa ng'ombe ulisababisha wimbi la utekaji nyara hivi karibuni katika jimbo la Katsina lililopo kaskazini magharibi mwa nchi. Wanafunzi wavulana zaidi ya 300 walitekwa nyara mapema mwezi huu lakini baadaye wakaachiliwa huru.

Mamlaka huko Katsina mwanzoni ililaumu utekaji nyara wa wavulana wa shule 344 kwa magenge ya majambazi ambao wamewateka nyara baadhi ya watu kwa ajili ya kulipwa fidia katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Halafu maafisa walibadilisha usemi wao , wakidai utekaji huo unahusiana na mzozo kati ya wafugaji ng'ombe na wakulima juu ya matumizi ya ardhi.

Lakini kamishna mstaafu wa polisi na mchambuzi wa usalama Lawrence Alobi hakubaliani na wazo hilo kwamba wafugaji walifanya shambulizi hilo.

"Wafugaji hawana shida yoyote na wakuu wa shule au wanafunzi. Shida yao iko kwa wakulima, mahali ambako wanaweza kulisha ng'ombe wao. Kwa hivyo, sijui uhusiano kati ya utekaji nyara wa wanafunzi hao na mivutano na wakulima.” alisema Alobi.

Kikundi cha wanamgambo wa Kiislam Boko Haram kilidai kuhusika na utekaji nyara wa wavulana hao wa shule na kutoa picha ya video inayoonyesha baadhi ya wavulana waliotekwa kabla ya kuachiliwa huru.

Madai hayo, ikiwa yatathibitishwa, yangeashiria mabadiliko kwa kundi hilo, ambalo hadi sasa limekuwa likifanya kazi hasa katika upande wa kaskazini mashariki mwa nchi.

Mtaalam wa usalama Kabir Adamu anasema anaamini utekaji nyara huo ulitekelezwa na majambazi walifanya hivyo kwa maagizo kutoka kwa kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar Shekau.

"Wito utakuwa umetolewa nae . Kilicho cha muhimu zaidi ni nani anayetoa maagizo. Kwa hivyo, ikiwa vikundi vya majambazi waliofanya mashambulizi wamejiweka chini ya mamlaka ya Shekau, basi inamaanisha ndiye yeye ambaye hatimaye aliyetoa maagizo.” Alisema Kabir.

Mizozo kati ya wafugaji ng'ombe na wakulima wa mazao imekuwepo nchini Nigeria kwa miaka mingi, na maelfu ya watu waliuwawa wakati wa mapigano makali ya ardhi kwa ajili ya malisho.

Chama cha wafugaji wa ng'ombe cha Miyetti Allah hakikuzungumza juu ya shutuma kutoka kwa polisi, lakini kikundi hicho kilishiriki katika kujadili kuachiliwa kwa wavulana wa shule.

Alobi anasema kulaumu mapigano ya wakulima na wafugaji kwa utekaji nyara kunaweza kutupilia mbali uwezekano wa kupanua msimamo mkali katika maeneo mengine ya nchi.

"Serikali inajaribu kutumia saikolojia ya watu ili kuwaondoa hofu, lakini nadhani serikali inapaswa kuwa ya kweli kwa watu ili kila kitu kitekelezwe kufuatana na hali halisi.”alisema Alobi.

Mamlaka nchini Nigeria mnamo mwaka 2016 ilitangaza kwamba kundi la Boko Haram limeshindwa na hivi karibuni lilikanusha madai ya kundi hilo hilo juu ya utekaji nyara, wakielezea kuwa ni minong'ono kutoka kwa farasi anayekufa. Lakini wataalam wa usalama watakuwa wakifuatilia hali hiyo kwa karibu ili kuona nini kitatokea baadaye.


Imeandaliwa na Sunday Shomari, VOA, Washington

XS
SM
MD
LG