Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken yupo Senegal kituo cha mwisho katika safari yake barani Afrika kuthibitisha tena ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili, wizara ya mambo ya nje Marekani ilisema mapema wiki hii.
Blinken alisema Jumamosi kwamba nchi yake inawekeza barani Afrika bila kuweka viwango vya madeni visivyo endelevu huku akishuhudia kusainiwa kwa mikataba yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni moja katika mji mkuu wa Senegal, Dakar.
Makubaliano hayo kati ya makampuni manne ya Marekani na Senegal ni sehemu ya nchi yake kuisaidia Afrika kujenga miundo mbinu kwa mikataba ya uwazi na endelevu. Blinken alikutana na Rais wa Senegal Macky Sall, katika makazi ya rais mapema leo Jumamosi mjini Dakar kuthibitisha tena ushirikiano wa karibu kati ya nchi zetu mbili kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Marekani.
Akiwa makini kutokosoa moja kwa moja miradi ya miundombinu ya China ambayo imeongezeka katika muongo mmoja uliopita Blinken alisema wakati wa ziara yake nchini Nigeria siku ya Ijumaa alibani kwamba mikataba ya kimataifa mara nyingi haieleweki na ni ya kulazimisha.
Marekani inawekeza bila kuitwisha nchi deni ambalo haiwezi kukabiliana nalo alisema wakati wa hafla ya utiaji saini na waziri wa uchumi wa Senegal, Amadou Hott. Mikataba hiyo itasaidia kuboresha miundombinu, kubuni nafasi za ajira, kuimarisha usalama wa umma, na uthabiti wa hali ya hewa, aliongeza.