Muasisi mwenza wa kampuni ya Microsoft, Bill Gates, ameeleza matumaini yake kwamba Nigeria itaweza kuushinda ugonjwa wa polio, licha ya changamoto kubwa zinazoifanya vigumu kuwachanja watoto katika baadhi ya maeneo.
Gates aliambia kipindi cha televisheni cha Sauti ya Amerika, Africa 54, siku ya Jumatano, kwamba visa viwili vipya vilivyoripotiwa hivi karibuni ni vya kuvunja moyo baada ya mafanikio makubwa katika juhudi za kupambana na ugonjwa huo, siyo tu barani Afrika, lakini pia huko Pakistan na Afghanistan, mataifa mawili pekee ambako polio bado ni janga.
Alisema changamoto kubwa ni kwamba kuna watoto ambao wataalamu wa afya wanapata shida kuwapata, na kuongeza kwamba itabidi kushirikiana hata Zaidi na serikali katika majimbo hayo , hususan Kaskazini Mashariki mwa jimbo la Borno.